Habakuki - Sura ya 1

Habakuki - Sura ya 1

1Ufunuo aliouona nabii Habakuki.

2Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa.

3Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.

4Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.

5Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa.

6Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao.

7Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe.

8Farasi zao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwa-mwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; huruka kama tai afanyaye haraka ale.

9Waja wote ili kufanya udhalimu; nyuso zao zimeelekezwa kwa bidii yao kama upepo wa mashariki, nao hukusanya mateka kama mchanga.

10Naam, huwadhihaki wafalme, na wakuu ni kitu cha kudharauliwa kwake; huidharau kila ngome; kwa maana hufanya chungu ya mavumbi, na kuitwaa.

11Kisha atapita kwa kasi, kama upepo, atapita na kuwa ana hatia; yeye ambaye nguvu zake ni mungu wake.

12Ee Bwana, Mungu wangu, mtakatifu wangu, wewe si wa milele? Hatutakufa. Ee Bwana, umemwandikia hukumu, nawe, Ee Jabali, umemweka imara ili aadhibishwe.

13Wewe uliye na macho safi hata usiweze kuangalia uovu, wewe usiyeweza kutazama ukaidi, mbona unawaangalia watendao kwa hila; na kunyamaza kimya, hapo mtu mwovu ammezapo mtu aliye mwenye haki kuliko yeye;

14na kufanya wanadamu kuwa kama samaki wa baharini, kama vitu vitambaavyo, ambavyo havina mtawala?

15Yeye huwatoa wote kwa ndoana yake, huwakamata katika wavu wake, na kuwakusanya katika juya lake; ndiyo sababu afurahi na kupendezwa.

16Kwa sababu hiyo huutolea wavu wake sadaka, na kulifukizia uvumba juya lake; kwa sababu kwa vitu vile fungu lake limenona, na chakula chake kimekuwa tele.

17Je! Atawatoa walio katika wavu wake, asiache kuwaua watu wa mataifa daima?