Habakuki - Sura ya 2

Habakuki - Sura ya 2

1Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu.

2Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.

3Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.

4Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.

5Naam, pamoja na hayo, divai ni mchumi mdanganyifu, mtu wa kiburi asiyekaa nyumbani mwake; huongeza tamaa yake kama kuzimu, naye huwa kama mauti, hawezi kushibishwa; bali hujikusanyia mataifa yote; hujiwekea kabila zote chungu chungu.

6Je! Hawa wote hawatapiga mfano juu yake, na mithali ya kusimanga juu yake, wakisema, Ole wake yeye aongezaye kisicho mali yake! Hata lini? Na ole wake yeye ajitwikaye mzigo wa rehani!

7Je! Hawatainuka ghafula wao watakaokuuma, hawataamka wao watakaokusumbua, nawe utakuwa mateka kwao?

8Kwa sababu umeteka nyara mataifa mengi, mabaki yote ya kabila watakuteka wewe; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake.

9Ole wake yeye aipatiaye nyumba yake mapato mabaya, ili apate kukiweka kioto chake juu, apate kujiepusha na mkono wa uovu!

10Wewe umeifanyia nyumba yako kusudi la aibu, kwa kukatilia mbali watu wengi, nawe umetenda dhambi juu ya roho yako.

11Kwa maana jiwe litapiga kelele katika ukuta, nayo boriti katika miti italijibu.

12Ole wake yeye ajengaye mji kwa damu, awekaye imara mji mkubwa kwa uovu!

13Angalieni; je! Jambo hili halikutoka kwa Bwana wa majeshi, kwamba watu wajishughulikie moto, na mataifa wajisumbue kwa ajili ya ubatili?

14Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Bwana, kama maji yaifunikavyo bahari.

15Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe utiaye sumu yako, na kumlevya pia, ili kuutazama uchi wao!

16Umejaa aibu badala ya utukufu; unywe nawe, uwe kama mtu asiyetahiriwa; kikombe cha mkono wa kuume wa Bwana kitageuzwa ukipokee, na aibu kuu itakuwa juu ya utukufu wako.

17Kwa maana udhalimu uliotendwa juu ya Lebanoni utakufunikiza, na kuangamizwa kwao wanyama kutakutia hofu; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake.

18Sanamu ya kuchora yafaa nini, hata yeye aliyeifanya ameichora? Sanamu ya kuyeyuka, nayo ni mwalimu wa uongo, yafaa nini, hata yeye aliyeifanya aiwekee tumaini lake, na kufanya sanamu zisizoweza kusema?

19Ole wake yeye auambiaye mti, Amka; aliambiaye jiwe lisiloweza kusema, Ondoka! Je! Kitu hicho kitafundisha? Tazama, kimefunikwa kwa dhahabu na fedha, wala hamna pumzi ndani yake kabisa.

20Lakini Bwana yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake.