Waebrania - Sura ya 11

Waebrania - Sura ya 11

1Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.

2Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa.

3Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.

4Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena.

5Kwa imani Henoko alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu.

6Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.

7Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake. Na hivyo akauhukumu makosa ulimwengu, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.

8Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.

9Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

10Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

11Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.

12Na kwa ajili ya hayo wakazaliwa na mtu mmoja, naye alikuwa kama mfu, watu wengi kama nyota za mbinguni wingi wao, na kama mchanga ulio ufuoni, usioweza kuhesabika.

13Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi.

14Maana hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe.

15Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea.

16Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji.

17Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee;

18naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa,

19akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.

20Kwa imani Isaka akawabariki Yakobo na Esau, hata katika habari ya mambo yatakayokuwa baadaye.

21Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.

22Kwa imani Yusufu, alipokuwa amekaribia mwisho wake, alitaja habari za kutoka kwao wana wa Israeli, akaagiza kwa habari ya mifupa yake.

23Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

24Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;

25akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;

26akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

27Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.

28Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao.

29Kwa imani wakapita kati ya Bahari ya Shamu, kama katika nchi kavu; Wamisri walipojaribu kufanya vivyo wakatoswa.

30Kwa imani kuta za Yeriko zikaanguka, zilipokwisha kuzungukwa siku saba.

31Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani.

32Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii;

33ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba,

34walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.

35Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora;

36wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;

37walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;

38(watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.

39Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;

40kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.