Waebrania - Sura ya 13

1Upendano wa ndugu na udumu.
2Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.
3Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mlivyo katika mwili.
4Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.
5Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.
6Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
7Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.
8Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.
9Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.
10Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiao ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake.
11Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi.
12Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango.
13Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake.
14Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.
15Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake.
16Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu.
17Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.
18Tuombeeni; maana tunaamini kwamba tuna dhamiri njema, tukitaka kuwa na mwenendo mwema katika mambo yote.
19Nami nawasihi zaidi sana kufanya hayo ili nirudishwe kwenu upesi.
20Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu,
21awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.
22Lakini nawasihi, ndugu, mchukuliane na neno hili lenye maonyo maana nimewaandikia kwa maneno machache.
23Jueni ya kuwa ndugu yetu Timotheo amekwisha kufunguliwa; ambaye, akija upesi, nitaonana nanyi pamoja naye.
24Wasalimuni wote wenye kuwaongoza, na watakatifu wote; hao walio wa Italia wanawasalimu.
25Neema na iwe nanyi nyote.