Waebrania - Sura ya 6

Waebrania - Sura ya 6

1Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu,

2na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele.

3Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.

4Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.

7Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki baraka zitokazo kwa Mungu;

8bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.

9Lakini, wapenzi, ijapokuwa twanena hayo, katika habari zenu tumesadiki mambo yaliyo mazuri zaidi, na yaliyo na wokovu.

10Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia.

11Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho;

12ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu.

13Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake,

14akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza.

15Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi.

16Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha.

17Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati;

18ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu;

19tuliyo nayo kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia,

20alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.