Isaya - Sura ya 14

Isaya - Sura ya 14

1Maana Bwana atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, naye atawaweka katika nchi yao wenyewe; na mgeni atajiunga nao, nao wataambatana na nyumba ya Yakobo.

2Na hao mataifa watawatwaa na kuwaleta mpaka mahali pao wenyewe, na nyumba ya Israeli watawamiliki, na kuwafanya watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana; nao watawachukua hali ya kufungwa watu wale waliowafunga wao, nao watawamiliki watu wale waliowaonea.

3Tena itakuwa katika siku ile, ambayo Bwana atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa;

4utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; Jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri!

5Bwana amelivunja gongo la wabaya, Fimbo ya enzi yao wenye kutawala.

6Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, Kwa mapigo yasiyokoma; Aliyewatawala mataifa kwa hasira, Ameadhibiwa asizuie mtu.

7Dunia yote inastarehe na kutulia; Hata huanzilisha kuimba.

8Naam, misunobari inakufurahia, Na mierezi ya Lebanoni, ikisema, Tokea wakati ulipolazwa chini wewe, Hapana mkata miti aliyetujia.

9Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako, Ili kukulaki utakapokuja; Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, Naam, walio wakuu wote wa dunia; Huwainua wafalme wote wa mataifa, Watoke katika viti vyao vya enzi.

10Hao wote watajibu na kukuambia, Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi!

11Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, Na sauti ya vinanda vyako; Funza wametandazwa chini yako, Na vidudu vinakufunika.

12Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!

13Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.

14Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.

15Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.

16Wao wakuonao watakukazia macho, Watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, Huyu ndiye aliyetikisa falme;

17Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?

18Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima, Kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe;

19Bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako, Kama chipukizi lililochukiza kabisa; Kama vazi la wale waliouawa, Wale waliochomwa kwa upanga, Wale washukao mpaka misingi ya shimo; Kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu.

20Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi, Kwa maana umeiharibu nchi yako, Umewaua watu wako; Kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele.

21Fanyeni tayari machinjo kwa watoto wake. Kwa sababu ya uovu wa baba zao; Wasije wakainuka na kuitamalaki nchi, Na kuujaza miji uso wa ulimwengu.

22Nami nitainuka, nishindane nao; asema Bwana wa majeshi; na katika Babeli nitang'oa jina na mabaki, mwana na mjukuu; asema Bwana.

23Tena nitaifanya hiyo nchi kuwa makao ya nungu, na maziwa ya maji; nami nitaifagilia mbali kwa ufagio wa uharibifu; asema Bwana wa majeshi.

24Bwana wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa; na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea;

25kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo nira yake iliyo juu yao itakapoondoka, na mzigo wake utatoka mabegani mwao.

26Hilo ndilo kusudi lililokusudiwa duniani mwote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote.

27Maana Bwana wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?

28Ufunuo huu ulikuja mwaka ule alipokufa mfalme Ahazi.

29Usifurahi, Ee Ufilisti, pia wote, Kwa sababu fimbo ile iliyokupiga imevunjika; Maana katika shina la nyoka atatoka fira, Na uzao wake ni joka la moto arukaye

30Nao walio maskini kabisa watakula, Na wahitaji watajilaza salama; Nami nitatia shina lako kwa njaa, Na mabaki yako watauawa.

31Piga yowe, Ee lango; lia, Ee mji; Ee Ufilisti, pia wote, umeyeyuka kabisa; Maana moshi unakuja toka kaskazini, Wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake.

32Wajumbe wa taifa hilo waletewe jibu gani? Ya kuwa Bwana ameiweka misingi ya Sayuni, na ndani yake wale walioonewa katika watu wake wataona kimbilio.