Isaya - Sura ya 16

Isaya - Sura ya 16

1Pelekeni wana-kondoo, kodi yake aitawalaye nchi toka Sela kuelekea jangwani, mpaka mlima wa binti Sayuni.

2Na binti za Moabu watakuwa kama ndege warukao huko na huko, kama kioto cha ndege waliotiwa hofu, kwenye vivuko vya Arnoni.

3Lete shauri; kata neno; fanya kivuli chako kuwa kama usiku kati ya mchana; wafiche waliofukuzwa; usiwachongee waliopotea.

4Watu wangu waliofukuzwa waache wakae pamoja nawe; katika habari za Moabu, uwe sitara kwake mbele ya uso wake anayeharibu; maana yeye atozaye kwa nguvu amekoma; afanyaye ukiwa ametoweka; waliokanyaga watu wametoka katika nchi.

5Na kiti cha enzi kitafanywa imara kwa rehema; na mmoja ataketi juu yake katika kweli, katika hema ya Daudi; akifanya hukumu, akitaka sana yaliyo haki, mwepesi wa kutenda haki.

6Tumesikia habari za kiburi cha Moabu, ya kwamba ni mwenye kiburi kingi; habari za majivuno yake, na kiburi chake, na ghadhabu yake; majivuno yake si kitu.

7Kwa sababu hiyo Moabu atalia kwa ajili ya Moabu, kila mmoja atalia, maana mtaiombolezea mikate ya zabibu ya Kir-Haresethi, mkipigwa sana.

8Maana makonde ya Heshboni yamenyauka, na mzabibu wa Sibma; mabwana wa mataifa wameyavunja matawi yake mateule; yamefika hata Yazeri, yalitanga-tanga hata nyikani; matawi yake yalitapakaa, yaliivuka bahari.

9Basi, naililia mizabibu ya Sibma kwa kilio cha Yazeri, nitawanyeshea machozi yangu, Ee Heshboni na Eleale, kwa kuwa kelele za vita zimeyaangukia mavuno ya matunda yako, na mavuno ya mizabibu yako.

10Na furaha imeondolewa, na shangwe toka mashamba yaliyozaa sana; hapana kuimba katika mashamba ya mizabibu, wala sauti za furaha; akanyagaye hakanyagi divai katika mashinikizo; nimeikomesha sauti ya furaha yake akanyagaye.

11Kwa sababu hiyo mtima wangu unamlilia Moabu kama kinubi, na matumbo yangu kwa ajili ya Kir-Heresi.

12Tena itakuwa, Moabu akionekana, na kujichosha kwa kulia juu ya mahali pa juu, na kuingia katika patakatifu pake aombe, hatapata kushinda.

13Hilo ndilo neno lile alilolisema Bwana juu ya Moabu zamani.

14Lakini sasa Bwana asema hivi, Katika muda wa miaka mitatu, kama miaka ya mtu wa mshahara, utukufu wa Moabu utadharauliwa, pamoja na wingi wake wote; mabaki yake yatakuwa machache sana, kama si kitu kabisa.