Isaya - Sura ya 2

Isaya - Sura ya 2

1Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu.

2Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi.

3Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu.

4Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.

5Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.

6Maana wewe umewaacha watu wako, nyumba ya Israeli, kwa sababu wamejaa kawaida za mashariki, nao ni wapiga ramli kama Wafilisti, na wanapana mikono na wana wa wageni.

7Tena nchi yao imejaa fedha na dhahabu, wala hapana mwisho wa hazina zao; tena nchi yao imejaa farasi, wala hapana mwisho wa magari yao.

8Tena nchi yao imejaa sanamu; huabudu kazi ya mikono yao, vitu vilivyofanywa kwa vidole vyao wenyewe.

9Mtu mnyonge huinama, na mtu mkubwa hujidhili; kwa hiyo usiwasamehe.

10Ingia ndani ya jabali; ukajifiche mavumbini mbele za utisho wa Bwana, mbele za utukufu wa enzi yake.

11Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye Bwana, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.

12Kwa maana kutakuwa siku ya Bwana wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini.

13Na juu ya mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani;

14na juu ya milima mirefu yote, na juu ya vilima vyote vilivyoinuka;

15na juu ya kila mnara mrefu, na juu ya kila ukuta ulio na boma;

16na juu ya merikebu zote za Tarshishi, na juu ya kila taswira ipendezayo.

17Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye Bwana, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.

18Nazo sanamu zitatoweka kabisa.

19Na watu wataingia ndani ya pango za majabali, na ndani ya mashimo ya nchi, mbele za utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia.

20Siku hiyo kila mtu atazitupilia mbali sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, walizojifanyia ili kuziabudu, kwa fuko na popo;

21ili aingie ndani ya pango za majabali, na ndani ya tundu za miamba iliyopasuka, mbele za utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia.

22Mwacheni mwanadamu ambaye pumzi yake i katika mianzi ya pua yake; kwa maana hudhaniwaje kuwa ni kitu?