Isaya - Sura ya 21

Isaya - Sura ya 21

1Ufunuo juu ya bara ya bahari. Kama tufani za Negebu

2Nimeonyeshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote.

3Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona.

4Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha.

5Wanaandika meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta.

6Maana Bwana ameniambia hivi, Enenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze.

7Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; asikilize sana, akijitahidi kusikiliza.

8Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu.

9Na, tazama, linakuja kundi la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili. Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini.

10Ewe niliyekufikicha, na nafaka ya sakafu yangu; Hayo niliyoyasikia kwa Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, nimewapasha habari zake.

11Ufunuo juu ya Duma. Mtu ananililia toka Seiri, Ee mlinzi, habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku?

12Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia; mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena.

13Ufunuo juu ya Arabuni. Ndani ya msitu wa Arabuni mtalala, Enyi misafara ya Wadedani.

14Waleteeni wenye kiu maji, Enyi wenyeji wa nchi ya Tema; Nendeni kuwalaki wakimbiao na chakula chao.

15Kwa maana wanakimbia mbele ya panga, Upanga uliofutwa, na upinde uliopindwa, Na mbele ya ukali wa vita.

16Kwa sababu Bwana ameniambia hivi, Katika muda wa mwaka, kama miaka ya mtu mwenye kuajiriwa, utaangamia utukufu wote wa Kedari.

17Na mabaki ya hesabu ya wavuta pinde, hao mashujaa wa Kedari watakuwa wachache; maana Bwana, Mungu wa Israeli, amenena neno hili.