Isaya - Sura ya 23

1Ufunuo juu ya Tiro. Toeni sauti za uchungu, enyi merikebu za Tarshishi, kwa maana umeharibika kabisa, hata hapana nyumba, hapana mahali pa kuingia; toka nchi ya Kitimu wamefunuliwa habari.
2Tulieni, enyi mkaao kisiwani; wewe ambaye wafanya biashara wa Sidoni, wavukao bahari, walikujaza.
3Vitu vilivyopandwa, vya Shihori, mavuno ya Nile, yaliyokuja juu ya maji mengi, ndiyo pato lake, naye alikuwa soko la mataifa.
4Tahayari, Ee Sidoni; kwa maana bahari imenena, hiyo ngome ya bahari ilisema, Sikuona utungu, wala sikuzaa, wala sikulea vijana, wala sikulea wanawali.
5Habari itakapofika Misri wataona uchungu sana kwa sababu ya habari ya Tiro.
6Piteni mpaka Tarshishi, enyi mkaao kisiwani, toeni sauti ya uchungu.
7Je! Huu ndio mji wenu wa furaha, ambao mwanzo wake ulikuwako tangu siku za kale, ambao miguu yake ilimchukua akae mbali sana?
8Ni nani aliyefanya shauri hili juu ya Tiro, uliotia watu taji, ambao wafanya biashara wake walikuwa wana wa wafalme, na wachuuzi wake ni watu wakuu wa dunia?
9Bwana wa majeshi ndiye aliyefanya shauri hili, ili kuharibu kiburi cha utukufu wote, na kuwaaibisha watu wa duniani wote pia.
10Pita katika nchi yako, kama Nile, Ee binti wa Tarshishi, hapana tena mshipi wa kukuzuia.
11Amenyosha mkono wake juu ya bahari, amezitikisa falme; Bwana ametoa amri katika habari za Kanaani, kuziangamiza ngome zake.
12Naye akasema, Usizidi kufurahi, ewe bikira uliyeaibishwa, binti wa Sidoni, haya, ondoka, uende hata Kitimu; huko nako hutapata raha.
13Tazama, nchi ya Wakaldayo; watu hao hawako tena; Mwashuri ameiweka tayari kwa hayawani wa jangwani; wamesimamisha buruji zao za vita, wameyaharibu majumba yake ya enzi, akaufanya kuwa uharibifu.
14Pigeni yowe, enyi merikebu za Tarshishi; maana ngome yenu imefanywa ukiwa.
15Basi, itakuwa katika siku ile, Tiro utasahauliwa miaka sabini, kadiri ya siku za mfalme mmoja; hata mwisho wa miaka sabini, Tiro utakuwa kama vile ulivyo wimbo wa kahaba.
16Twaa kinubi, tembea mjini, Ewe kahaba uliyesahauliwa; Piga vizuri, imba nyimbo nyingi, Upate kukumbukwa tena.
17Hata itakuwa mwisho wa miaka sabini, Bwana ataizuru nchi ya Tiro, naye atarudi apate ujira wake, atafanya ukahaba pamoja na falme zote za ulimwengu juu ya uso wa dunia.
18Na biashara yake na ujira wake utakuwa wakfu kwa Bwana, hautawekwa hazinani wala hautawekwa akiba; bali mapato ya biashara yake yatakuwa mali zao wakaao mbele za Bwana, wapate kula na kushiba, na kuvaa mavazi ya fahari.