Isaya - Sura ya 26
1Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma.
2Wekeni wazi malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie.
3Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.
4Mtumainini Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele.
5Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini.
6Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji.
7Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki.
8Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee Bwana; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako.
9Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki.
10Mtu mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa Bwana.
11Bwana, mkono wako umeinuliwa, lakini hawaoni; lakini watauona wivu wako kwa ajili ya watu wako, nao watatahayari; naam, moto utawala adui zako.
12Bwana, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote.
13Ee Bwana, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametumiliki; lakini kwa msaada wako peke yako tutalitaja jina lako.
14Wao wamekufa, hawataishi; wamekwisha kufariki, hawatafufuka; kwa sababu hiyo umewajilia, na kuwaangamiza, na kuupoteza ukumbusho wao.
15Umeliongeza hilo taifa, Bwana, umeliongeza taifa; wewe umetukuzwa, umeipanua mipaka yote ya nchi hii.
16Bwana, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao.
17Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na utungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee Bwana.
18Tumekuwa na mimba, tumekuwa na utungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wo wote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani.
19Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.
20Njoni, watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita.
21Kwa maana, tazama, Bwana anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao; ardhi nayo itafunua damu yake, wala haitawafunika tena watu wake waliouawa.

Swahili
Italiano (it-IT)
Português do Brasil (pt-BR)
Polski (PL)
Deutsch (Deutschland)
Français (France)
Español (España)
Українська Біблія у перекладі Огієнка
English Bible - 21ST CENTURY KING JAMES (KJ21)