Isaya - Sura ya 27

Isaya - Sura ya 27

1Katika siku hiyo Bwana, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye kuzonga-zonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.

2Katika siku hiyo; Shamba la mizabibu la mvinyo, liimbieni.

3Mimi, Bwana, nalilinda, Nitalitia maji kila dakika, Asije mtu akaliharibu; Usiku na mchana nitalilinda.

4Hasira sinayo ndani yangu; Kama mibigili na miiba ingekuwa mbele zangu, Ningepanga vita juu yake, Ningeiteketeza yote pamoja.

5Au azishike nguvu zangu, Afanye amani nami; Naam, afanye amani nami.

6Siku zijazo Yakobo atatia mizizi; Israeli atatoa maua na kuchipuka; Nao watajaza uso wa ulimwengu matunda.

7Je! Amempiga kama hilo pigo la hao waliompiga, au ameuawa kama walivyouawa wao waliouawa na yeye?

8Umemwadhibu kwa kiasi, ulipomfukuza; ukampepeta kwa upepo mkali katika siku ya upepo wa mashariki.

9Basi, uovu wa Yakobo utatakaswa hivyo, na hayo ndiyo matunda yote ya kumwondolea dhambi yake; afanyapo mawe yote ya madhabahu kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa, hata maashera na sanamu za jua havitasimama tena.

10Kwa maana mji ulio na boma umekuwa peke yake, makao yaliyoachwa na ukiwa kama jangwa; huko ndiko atakakolisha ndama, na huko ndiko atakakolala, na kuyala matawi yake.

11Matawi yake yatakapokauka yatavunjwa; wanawake watakuja na kuyachoma moto; kwa maana hawa si watu wenye akili; kwa sababu hiyo yeye aliyewaumba hatawahurumia, yeye aliyewafanya hatawasamehe.

12Tena itakuwa katika siku hiyo, Bwana atayapiga-piga matunda yake toka gharika ya Mto hata kijito cha Misri, nanyi mtakusanywa mmoja mmoja, enyi wana wa Israeli.

13Tena itakuwa katika siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa, nao waliokuwa karibu na kuangamia katika nchi ya Ashuru watakuja; na hao waliotupwa katika nchi ya Misri; nao watamsujudu Bwana katika mlima mtakatifu huko Yerusalemu.