Isaya - Sura ya 33

1Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.
2Ee Bwana, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu
3Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako.
4Na mateka yako yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige.
5Bwana ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.
6Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba.
7Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.
8Njia kuu zimeachwa, msafiri amekoma; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu.
9Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani.
10Basi, sasa nitasimama; asema Bwana; sasa nitajiinua, sasa nitajitukuza.
11Ninyi mtachukua mimba ya makapi, mtazaa majani makavu; pumzi yenu ni moto utakaowateketeza wenyewe.
12Nao mataifa watakuwa kama kuchoma chokaa, kama miiba iliyokatika, iteketezwayo motoni.
13Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu.
14Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?
15Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu.
16Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.
17Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana.
18Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara?
19Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo.
20Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang'olewa, wala kamba zake hazitakatika.
21Bali huko Bwana atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo.
22Kwa maana Bwana ndiye mwamuzi wetu; Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa.
23Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka.
24Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.