Isaya - Sura ya 38

Isaya - Sura ya 38

1Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.

2Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana,

3akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.

4Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema,

5Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.

6Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.

7Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kuwa Bwana atalitimiza jambo hili alilolisema;

8Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.

9Haya ndiyo maandiko ya Hezekia, mfalme wa Yuda, alipokuwa hawezi, naye akapona ugonjwa wake.

10Nalisema, Katika usitawi wa siku zangu nitakwenda kuingia malango ya kuzimu; Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.

11Nalisema, Sitamwona Bwana, yeye Bwana, katika nchi ya walio hai; Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao wakaao duniani.

12Kao langu limeondolewa kabisa, limechukuliwa kama hema ya mchungaji; Nimekunja maisha yangu kama mfumaji; atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi; Tangu mchana hata usiku wanimaliza.

13Nalijituliza hata asubuhi; kama simba, aivunja mifupa yangu yote; Tangu mchana hata usiku wanimaliza.

14Kama mbayuwayu au korongo ndivyo nilivyolia; Naliomboleza kama hua; macho yangu yamedhoofu kwa kutazama juu; Ee Bwana, nimeonewa, na uwe mdhamini wangu.

15Niseme nini? Yeye amenena nami, na yeye mwenyewe ametenda hayo; Nitakwenda polepole miaka yangu yote, kwa sababu ya uchungu wa nafsi yangu.

16Ee Bwana, kwa mambo hayo watu huishi; Na uhai wa roho yangu u katika hayo yote; Kwa hiyo uniponye na kunihuisha.

17Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa na shimo la uharibifu; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.

18Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako.

19Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo; Baba atawajulisha watoto kweli yako.

20Bwana yu tayari kunipa wokovu. Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu, Siku zote za maisha yetu nyumbani mwa Bwana.

21Maana Isaya amesema, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.

22Tena Hezekia alikuwa amesema, Iko ishara gani ya kunionyesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa Bwana?