Isaya - Sura ya 40

1Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu.
2Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana adhabu maradufu kwa dhambi zake zote.
3Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.
4Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa;
5Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.
6Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye, Lia! Nikasema, Nilie nini? Wote wenye mwili ni majani, Na wema wake wote ni kama ua la kondeni;
7Majani yakauka, ua lanyauka; Kwa sababu pumzi ya Bwana yapita juu yake. Yakini watu hawa ni majani.
8Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele.
9Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, Panda juu ya mlima mrefu; Wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, Paza sauti kwa nguvu; Paza sauti yako, usiogope; Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu.
10Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na ijara yake i mbele zake.
11Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.
12Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiri mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani?
13Ni nani aliyemwongoza roho ya Bwana, na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake?
14Alifanya shauri na nani, ni nani aliyemwelimisha na kumfunza njia ya hukumu, na kumfunza maarifa, na kumwonyesha njia ya fahamu?
15Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama ni kitu kidogo sana.
16Lebanoni nayo hautoshi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara.
17Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake; huhesabiwa kwake kuwa duni ya si kitu, na ubatili.
18Basi, mtamlinganisha Mungu na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani?
19Sanamu fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha.
20Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi mstadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika.
21Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia?
22Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa;
23ndiye awatanguaye wakuu, na kuwabatilisha waamuzi wa dunia.
24Naam, hawakupandwa; hawakutiwa katika ardhi kama mbegu; naam, shina lao halikutia mizizi katika ardhi; tena awapuzia tu, wakanyauka, upepo wa kisulisuli wawaondoa kama mabua makavu.
25Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu.
26Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.
27Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie?
28Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.
29Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.
30Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;
31bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.