Isaya - Sura ya 43

Isaya - Sura ya 43

1Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.

2Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.

3Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.

4Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.

5Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;

6nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia.

7Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.

8Walete vipofu walio na macho, na viziwi walio na masikio.

9Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonyesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli.

10Ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine.

11Mimi, naam, mimi, ni Bwana, zaidi yangu mimi hapana mwokozi.

12Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, nami ni Mungu.

13Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?

14Bwana, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia.

15Mimi ni Bwana, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu.

16Bwana asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu;

17atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi.

18Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.

19Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.

20Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu;

21watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.

22Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli.

23Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani.

24Hukuninunulia manukato kwa fedha, wala hukunishibisha kwa mafuta ya sadaka zako; bali umenitumikisha kwa dhambi zako, umenichosha kwa maovu yako.

25Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.

26Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.

27Baba yako wa kwanza alifanya dhambi, na wakalimani wako wameniasi.

28Kwa hiyo nitawatia unajisi wakuu wa patakatifu, nami nitamfanya Yakobo kuwalaani, na Israeli kuwa tukano.