Isaya - Sura ya 55

Isaya - Sura ya 55

1Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani.

2Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono.

3Tegeni masikio yenu, na kunijia; Sikieni, na nafsi zenu zitaishi; Nami nitafanya nanyi agano la milele, Naam, rehema za Daudi zilizo imara.

4Angalieni, nimemweka kuwa shahidi kwa kabila za watu; kuwa kiongozi na jemadari kwa kabila za watu.

5Tazama, utaita taifa usilolijua, na taifa lisilokujua wewe litakukimbilia, kwa sababu ya Bwana, Mungu wako, na kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli; maana amekutukuza.

6Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu;

7Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.

8Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.

9Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

10Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula;

11ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.

12Maana mtatoka kwa furaha, Mtaongozwa kwa amani; Mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi.

13Badala ya michongoma utamea msunobari, Na badala ya mibigili, mhadesi; Jambo hili litakuwa la kumpatia Bwana jina, Litakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali.