Isaya - Sura ya 57

Isaya - Sura ya 57

1Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya.

2Yeye huingia katika amani; wao hustarehe katika vitanda vyao, kila mtu aendaye katika unyofu wake.

3Lakini ninyi karibuni hapa, enyi wana wa mwanamke mchawi, uzao wa mzinzi na kahaba.

4Mnafanya dhihaka yenu juu ya nani? Mmepanua vinywa vyenu, na kutoa ndimi zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo;

5ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi; ninyi mnaoua watoto mabondeni, chini ya mianya ya majabali?

6Sehemu yako i katika makokoto ya bonde; hayo ndiyo kura yako; umeyamwagia hayo sadaka ya kinywaji, umeyatolea sadaka ya unga; je! Niwe radhi na mambo hayo?

7Umeweka kitanda chako juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; ukaenda huko ili kutoa dhabihu.

8Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako; kwa maana umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona.

9Ulimwendea mfalme na mafuta ya marhamu, ukaongeza manukato yako, ukawatuma wajumbe wako waende mbali, ukajidhili sana hata kuzimu.

10Ulikuwa umechoka kwa ajili ya urefu wa njia yako; lakini hukusema, Hapana matumaini; ulipata kuhuishwa nguvu zako; kwa sababu hiyo hukuugua.

11Tena ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo, wala hukunikumbuka mimi, wala kuweka hayo moyoni? Je! Mimi sikunyamaza tangu zamani, hata huniogopi?

12Mimi nitatangaza haki yako, na matendo yako hayatakufaa.

13Utakapolia, na wakuponye hao uliowakusanya; lakini upepo utawachukua; uvuvio tu utawachukulia mbali; lakini yeye anayenitumaini ataimiliki nchi, na kuurithi mlima wangu mtakatifu.

14Naye atasema, Tutieni, tutieni, Itengenezeni njia, Kiondoeni kila kikwazacho Katika njia ya watu wangu.

15Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.

16Kwa kuwa sitashindana na watu siku zote, wala sitakuwa na hasira siku zote; maana roho ingezimia mbele zangu, na hizo nafsi nilizozifanya.

17Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake naliona hasira, nikampiga; nalificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe.

18Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia.

19Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; asema Bwana; nami nitamponya.

20Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka.

21Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu.