Isaya - Sura ya 64

Isaya - Sura ya 64

1Laiti ungepasua mbingu, na kushuka, ili milima iteteme mbele zako;

2kama vile moto uchomapo vichaka, na moto uchemshapo maji; ili kuwajulisha adui zako jina lako, mataifa wakatetemeke mbele zako!

3Ulipofanya mambo ya kutisha tusiyoyatazamia, ulishuka, milima ikatetema mbele zako.

4Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe, atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye.

5Wewe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo haki na kuyatenda, watu wale wakukumbukao katika njia zako; tazama, ulikuwa na hasira, nasi tulitenda dhambi; tumekuwa katika mambo haya muda mwingi; nasi, je! Tutaokolewa?

6Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.

7Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu.

8Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.

9Ee Bwana, usione hasira nyingi, wala usiukumbuke uovu siku zote; tazama, angalia, twakusihi, sisi sote tu watu wako.

10Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa, Sayuni umekuwa jangwa, Yerusalemu umekuwa ukiwa.

11Nyumba yetu takatifu, nzuri, walimokusifu baba zetu, imeteketea moto; vitu vyetu vyote vyenye kupendeza vimeharibika.

12Utajizuia usiyaangalie mambo haya, Ee Bwana? Utanyamaza, na kututesa sana?