Yeremia - Sura ya 2

Yeremia - Sura ya 2

1Neno la Bwana likanijia, kusema,

2Enenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Nakukumbuka, hisani ya ujana wako, upendo wa wakati wa uposo wako; Jinsi ulivyonifuata huko jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu.

3Israeli walikuwa utakatifu kwa Bwana; malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu utawajilia; asema Bwana.

4Lisikieni neno la Bwana, ninyi nyumba ya Yakobo, na ninyi, jamaa zote za nyumba ya Israeli.

5Bwana asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili?

6Wala hawakusema, Yuko wapi Bwana, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani, katika nchi ya ukame na mashimo, katika nchi ya kiu na ya kivuli cha mauti, katika nchi ambayo ndani yake hapiti mtu, wala haikukaliwa na watu?

7Nami nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo.

8Makuhani hawakusema, Yuko wapi Bwana? Wala wana-sheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu.

9Basi, kwa ajili ya hayo nitateta nanyi, asema Bwana, nami nitateta na watoto wa watoto wenu.

10Maana, vukeni mpaka visiwa vya Kitimu, mkaone; tumeni watu waende Kedari, mkafikiri sana; mkaone kwamba jambo kama hili limekuwa wakati wo wote.

11Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia.

12Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana.

13Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.

14Je! Israeli ni mtumwa? Je! Ni mzalia? mbona amekuwa mateka?

15Wana-simba wamenguruma juu yake, wametoa sana sauti zao; Nao wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketea, haina watu.

16Tena wana wa Nofu na Tahpanesi wamevunja utosi wa kichwa chako.

17Je! Hukujipatia mambo haya mwenyewe, kwa kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, alipokuongoza njiani?

18Na sasa una nini utakayotenda katika njia iendayo Misri, kunywa maji ya Shihori? Au una nini utakayotenda katika njia iendayo Ashuru, kunywa maji ya ule Mto?

19Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, Bwana wa majeshi.

20Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba.

21Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu?

22Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU.

23Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake;

24punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? Wote wamtafutao hawatajichokesha nafsi zao; katika mwezi wake watamwona.

25Zuia mguu wako usikose kiatu, na koo yako isiwe na kiu; lakini wewe ulisema, Hapana matumaini kabisa; la, maana nimewapenda wageni, nami nitawafuata.

26Kama mwivi aonavyo haya akamatwapo, ndivyo waonavyo haya nyumba ya Israeli; wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao;

27waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe.

28Lakini wako wapi miungu yako ulioifanya? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda.

29Mbona mnataka kuteta nami? Ninyi nyote mmeniasi, asema Bwana.

30Nimewapiga watoto wako bure; hawakukubali kurudiwa; upanga wenu wenyewe umewala manabii wako, kama simba aharibuye.

31Ee kizazi litazameni neno la Bwana. Je! Nimekuwa jangwa kwa Israeli? Au nchi yenye giza kuu? Mbona watu wangu wanasema, Sisi tumetoroka, hatutaki kuja kwako tena?

32Je! Mwanamwali aweza kusahau mapambo yake, au bibi arusi mavazi yake? Lakini watu wangu wamenisahau mimi kwa muda wa siku zisizo na hesabu.

33Jinsi ulivyoitengeneza njia yako ili kutafuta mapenzi! Kwa sababu hiyo hata wanawake wabaya umewafundisha njia zako.

34Tena katika pindo za nguo zako imeonekana damu ya roho zao maskini wasio na hatia; sikuiona penye mahali palipobomoka, lakini naliiona juu ya hawa wote.

35Lakini ulisema, Sina hatia mimi; bila shaka hasira yake imegeuka na kuniacha. Tazama, nitaingia hukumuni pamoja nawe, kwa sababu unasema, Sikutenda dhambi mimi.

36Mbona unatanga-tanga hivi upate kugeuza mwendo wako? Utaona haya kwa ajili ya Misri pia, kama ulivyoona haya kwa ajili ya Ashuru.

37Hata kwake pia utatoka, na mikono yako juu ya kichwa chako; kwa maana Bwana amewakataa uliowakimbilia, wala hutafanikiwa katika hao.