Yeremia - Sura ya 22

Yeremia - Sura ya 22

1Bwana akasema hivi, Shuka nyumbani kwa mfalme wa Yuda, ukaseme neno hili huko,

2ya kwamba, Sikia neno la Bwana, Ee mfalme wa Yuda; wewe uketiye katika kiti cha enzi cha Daudi, wewe, na watumishi wako, na watu wako wote waingiao kwa malango haya;

3Bwana asema hivi, Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa.

4Kwa maana mkifanya haya kweli kweli, ndipo watakapoingia kwa malango ya nyumba hii wafalme wenye kuketi katika kiti cha enzi cha Daudi, wanakwenda kwa magari, na wamepanda farasi yeye, na watumishi wake, na watu wake.

5Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa.

6Kwa maana Bwana asema hivi, katika habari ya nyumba ya mfalme wa Yuda; Wewe u Gileadi kwangu, na kichwa cha Lebanoni; Ila hakika nitakufanya kuwa jangwa, na miji isiyokaliwa na watu.

7Nami nitakufanyia tayari watu wenye kuharibu, kila mtu na silaha zake; Nao watakata mierezi miteule yako, na kuitupa motoni.

8Na mataifa mengi watapita karibu na mji huu, nao watasema kila mtu na jirani yake, Nini maana yake Bwana kuutenda hivi mji huu mkubwa?

9Ndipo watakapojibu, Ni kwa sababu waliliacha agano la Bwana, Mungu wao, wakaabudu miungu mingine, na kuitumikia.

10Msimlilie aliyekufa, wala msimwombolezee, Bali mlilieni huyo aendaye zake mbali; Kwa maana yeye hatarudi tena, Wala hataiona nchi aliyozaliwa.

11Maana Bwana asema hivi, katika habari za Shalumu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; aliyemiliki badala ya Yosia, baba yake, yeye aliyetoka mahali hapa; Hatarudi huku tena;

12bali katika mahali pale walipomchukua mateka ndipo atakapokufa, wala hataiona nchi hii tena kamwe.

13Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu! Na vyumba vyake kwa udhalimu! Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira, Wala hampi mshahara wake;

14Asemaye, Nitajijengea nyumba pana na vyumba vipana; Naye hujikatia madirisha; Na kuta zake zimefunikwa kwa mierezi, Na kupakwa rangi nyekundu.

15Je! Utatawala kwa sababu unashindana na watu kwa mierezi? Baba yako, je! Hakula na kunywa, na kufanya hukumu na haki? Hapo ndipo alipofanikiwa.

16Alihukumu maneno ya maskini na mhitaji; hapo ndipo alipofanikiwa. Je! Huku siko kunijua, asema Bwana?

17Bali macho yako na moyo wako hauna utakalo ila kutamani, na kumwaga damu isiyo na hatia, na kudhulumu, na kutenda jeuri.

18Basi, Bwana asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake.

19Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.

20Haya panda Lebanoni, ukalie Upalize sauti yako katika Bashani; Ukalie kutoka Abarimu; Maana wapenzi wako wote wameangamia.

21Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema, Sitaki kusikia. Hii ndiyo iliyokuwa desturi yako tangu ujana wako, kutokuitii sauti yangu.

22Upepo utawalisha wachungaji wako wote, na wapenzi wako watakwenda kufungwa; hakika wakati huo utatahayarika, na kufadhaika kwa sababu ya uovu wako wote.

23Wewe ukaaye Lebanoni, Ufanyaye kioto chako katika mierezi, Utakuwa na hali ya kuhurumiwa sana, Upatapo utungu kama wa mwanamke azaaye.

24Kama niishivyo mimi, asema Bwana, hata Konia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, angekuwa pete yenye muhuri katika mkono wangu wa kuume, ningekung'oa wewe hapo;

25nami nitakutia katika mikono ya watu wale wakutafutao roho yako, na katika mikono yao unaowaogopa, naam, katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya Wakaldayo.

26Nami nitakutupa nje, wewe na mama yako aliyekuzaa, mwende nchi nyingine ambayo hamkuzaliwa huko, nanyi mtakufa huko.

27Lakini nchi ile ambayo wanatamani kuirudia, hawatairudia kamwe.

28Je! Mtu huyu, Konia, ni chombo kilichodharauliwa, na kuvunjika? Ni chombo kisichopendeza? Mbona wametupwa, yeye na wazao wake, na kutupwa katika nchi wasiyoijua?

29Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la Bwana.

30Bwana asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda.