Yeremia - Sura ya 3

Yeremia - Sura ya 3

1Watu husema, Mtu akimwacha mkewe, naye akienda zake, akawa mke wa mtu mwingine, je! Mtu huyo atamrudia tena? Je! Nchi hiyo haitatiwa unajisi? Lakini wewe umefanya mambo ya ukahaba na wapenzi wengi; nawe, je! Utanirudia mimi? Asema Bwana.

2Inua macho yako, ukavitazame vilele vya milima, ukaone; pa wapi mahali ambapo hawakulala nawe? Kando ya njia umeketi ili kuwangojea, kama vile Mwarabu jangwani; nawe umeitia nchi unajisi kwa ukahaba wako na uovu wako.

3Kwa sababu hiyo manyunyu yamezuiliwa, wala hapakuwa na mvua ya vuli; hata hivyo ulikuwa na kipaji cha uso cha kahaba, ulikataa kutahayarika.

4Je, tokea wakati huu hutanililia, Ee Baba yangu, wewe u kiongozi wa ujana wangu?

5Je! Ataishika hasira yake hata milele? Ataishika hata mwisho? Tazama, umesema hivyo, bali umetenda mambo mabaya, umefuata njia yako mwenyewe.

6Tena, Bwana akaniambia siku za mfalme Yosia, Je! Umeyaona aliyotenda Israeli mwenye kuasi? Amepanda juu ya kila mlima mrefu, akafanya huko mambo ya ukahaba, tena, chini ya kila mti wenye majani mabichi.

7Nami nalisema baada ya yeye kuyatenda hayo yote, Atanirudia mimi, lakini hakurudi; na dada yake, Yuda mwenye hiana, akayaona hayo.

8Nami nikaona, wakati nilipokuwa nimemwacha Israeli mwenye kuasi, nikampa hati ya talaka kwa sababu hiyo ya kuzini, dada yake, Yuda mwenye hiana, hakufanya hofu; bali yeye naye akaenda akafanya mambo ya ukahaba.

9Hata ikawa, kwa sababu alikuwa mwepesi wa kufanya ukahaba, nchi ikatiwa unajisi, naye akazini na mawe na miti.

10Na pamoja na hayo yote dada yake, Yuda mwenye hiana, hajanirudia mimi kwa moyo wake wote, bali kwa unafiki, asema Bwana.

11Bwana, akaniambia, Israeli mwenye kuasi amejionyesha kuwa mwenye haki kuliko Yuda mwenye hiana.

12Enenda, ukatangaze maneno haya kuelekea upande wa kaskazini, ukaseme, Rudi, Ee Israeli mwenye kuasi, asema Bwana; sitakutazama kwa hasira; maana mimi ni mwenye rehema, asema Bwana, sitashika hasira hata milele.

13Ungama uovu wako tu; ya kwamba umemwasi Bwana, Mungu wako, na njia zako zimekuwa nyingi kuwaendea wageni chini ya kila mti wenye majani mabichi, wala hamkuitii sauti yangu, asema Bwana.

14Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema Bwana; maana mimi ni mume wenu; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni;

15nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu.

16Kisha itakuwa, mtakapoongezeka na kuwa wengi katika nchi hiyo, asema Bwana, siku zile hawatasema tena, Sanduku la agano la Bwana; wala halitaingia moyoni; wala hawatalikumbuka, wala hawatalizuru, wala hayatafanyika hayo tena.

17Wakati ule watauita Yerusalemu kiti cha enzi cha Bwana; na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la Bwana; wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbaya.

18Siku zile nyumba ya Yuda watakwenda pamoja na nyumba ya Israeli, nao watakuja pamoja, kutoka nchi ya kaskazini, mpaka nchi ile niliyowapa baba zenu iwe urithi wao.

19Lakini mimi nalisema, Nitawezaje kukuweka pamoja na watoto, na kukupa nchi ipendezayo, urithi ulio mwema wa mataifa? Nami nikasema, Mtaniita, Baba yangu, wala hamtageuka na kuacha kunifuata.

20Hakika kama vile mke amwachavyo mumewe kwa hiana, ndivyo mlivyonitenda mimi kwa hiana, Ee nyumba ya Israeli, asema Bwana.

21Sauti inasikiwa juu ya vilele vya milima, ni kulia kwao na maombi yao wana wa Israeli; kwa kuwa wameipotosha njia yao, wamemsahau Bwana, Mungu wao.

22Rudini, enyi watoto waasi, mimi nitaponya maasi yenu. Tazama, tumekuja kwako; maana wewe u Bwana, Mungu wetu.

23Ni kweli, msaada haufai unaotazamiwa kutoka milimani, makutano yenye mshindo juu ya milima; ni kweli, wokovu wa Israeli ni katika Bwana, Mungu wetu.

24Lakini kitu cha aibu kimeila kazi ya baba zetu tokea ujana wetu; makundi yao ya kondoo na ng'ombe, wana wao na binti zao.

25Na tulale kwa aibu yetu, haya yetu na itufunike; kwa maana tumemwasi Bwana, Mungu wetu, sisi na baba zetu, tangu ujana wetu hata leo; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu.