Yeremia - Sura ya 30

Yeremia - Sura ya 30

1Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,

2Bwana Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Uyaandike kitabuni maneno hayo yote niliyokuambia.

3Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapowarejeza watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa, asema Bwana; nami nitawarudisha hata nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki.

4Na haya ndiyo maneno aliyosema Bwana, katika habari za Israeli, na katika habari za Yuda.

5Maana Bwana asema hivi, Tumesikia sauti ya tetemeko, na ya hofu, wala si ya amani.

6Ulizeni sasa, mkaone kwamba mwanamume aona utungu wa uzazi; mbona, basi, ninaona kila mtu anaweka mikono yake viunoni, kama mwanamke aliye na utungu, na nyuso zote zimegeuka rangi.

7Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo.

8Na itakuwa katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, nitaivunja nira yake itoke shingoni mwako, nami nitavipasua vifungo vyako; wala wageni hawatamtumikisha tena;

9bali watamtumikia Bwana, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao.

10Kwa sababu hiyo usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema Bwana; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu.

11Maana mimi ni pamoja nawe, asema Bwana, nikuokoe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokutawanya, bali sitakukomesha wewe kabisa; lakini nitakurudi kwa hukumu, wala sitakuacha bila adhabu.

12Maana Bwana asema hivi, Maumivu yako hayaponyekani, na jeraha yako ni kubwa.

13Hapana mtu wa kukutetea; kwa jeraha yako huna dawa ziponyazo.

14Wote wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha ya adui, kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zilikuwa zimeongezeka.

15Mbona unalilia maumivu yako? Hayaponyeki maumivu yako; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zimeongezeka, nimekutenda haya.

16Basi, watu wote wakulao wataliwa; na adui zako wote watakwenda kufungwa; kila mmoja wao; na hao waliokuteka nyara watatekwa; na wote waliokuwinda nitawafanya kuwa mawindo.

17Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.

18Bwana asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake.

19Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge.

20Watoto wao nao watakuwa kama zamani, na kusanyiko lao litathibitika mbele zangu, nami nitawaadhibu wote wawaoneao.

21Na mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo wa kuthubutu kunikaribia? Asema Bwana.

22Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

23Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea tufani ya kudumu; itawaangukia waovu vichwani.

24Hasira kali ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kutenda, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtayafahamu haya.