Yeremia - Sura ya 38

Yeremia - Sura ya 38

1Na Shefatia, mwana wa Matani, na Gedalia, mwana wa Pashuri, na Yukali, mwana wa Shelemia, na Pashuri, mwana wa Malkiya, wakayasikia maneno ambayo Yeremia aliwaambia watu wote, kusema,

2Bwana asema hivi, Akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atokaye kwenda kwa Wakaldayo ataishi, naye atapewa maisha yake yawe kama nyara, naye ataishi.

3Bwana asema hivi, Bila shaka mji huu utatiwa katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, naye atautwaa.

4Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari.

5Naye mfalme Sedekia akasema, Tazama, yu mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lo lote kinyume chenu.

6Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo.

7Basi, Ebedmeleki, Mkushi, towashi, aliyekuwa katika nyumba ya mfalme, aliposikia kama wamemtia Yeremia shimoni; na wakati huo mfalme alikuwa amekaa katika lango la Benyamini;

8Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema,

9Ee bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji.

10Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, Chukua pamoja nawe watu thelathini toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa.

11Basi Ebedmeleki akawachukua watu hao pamoja naye, akaingia ndani ya nyumba ya mfalme chini ya ghala, akatoa mle nguo zilizotupwa, na vitambaa vikuukuu, akamtelemshia Yeremia shimoni kwa kamba.

12Naye Ebedmeleki, Mkushi, akamwambia Yeremia, Tia nguo hizi zilizotupwa, na vitambaa hivi vikuukuu, chini ya kamba kwapani. Naye Yeremia akafanya hivyo.

13Basi wakamwinua Yeremia kwa kamba hizo, wakamtoa shimoni; naye Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi.

14Kisha mfalme Sedekia akatuma watu, akamleta nabii Yeremia kwake, ndani ya maingilio ya tatu ya nyumba ya Bwana; mfalme akamwambia Yeremia, Nataka kukuuliza neno, nawe usinifiche neno lo lote.

15Basi Yeremia akamwambia Sedekia, Kama nikikufunulia neno hilo, je! Hutaniua wewe? Tena, mimi nikikupa shauri wewe hutanisikiliza.

16Basi Sedekia mfalme akamwapia Yeremia kwa siri, akisema, Kama Bwana aishivyo, yeye aliyetufanyia roho zetu, sitakuua, wala sitakutia katika mikono ya watu hao wanaokutafuta wakuue.

17Ndipo Yeremia akamwambia Sedekia, Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama ukitoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi nafsi yako utaishi, wala mji huu hautateketezwa; nawe utaishi na nyumba yako;

18bali ukikataa kutoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi, mji huu utatiwa katika mikono ya Wakaldayo nao watauteketeza, hata na wewe hutajiepusha na mikono yao.

19Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, Nawaogopa Wayahudi waliowakimbilia Wakaldayo, wasije wakanitia katika mikono yao, nao wakanidhihaki.

20Lakini Yeremia akasema, La! Hawatakutoa. Nakusihi, uitii sauti ya Bwana katika hayo ninayokuambia; ndivyo itakavyokufaa, na nafsi yako utaishi.

21Lakini kama ukikataa kutoka, hili ndilo neno ambalo Bwana amenionyesha;

22Tazama, wanawake wote, walioachwa ndani ya nyumba ya mfalme wa Yuda, watatolewa na kuchukuliwa kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, na wanawake hao watasema, Rafiki zako walio karibu wamekudanganya, nao wamekushinda; na kwa kuwa miguu yako imezama matopeni sasa, wamegeuka na kurudi nyuma.

23Na watawatoa wake zako, na watoto wako wote, na kuwachukua kwa Wakaldayo; wala wewe hutapona na mikono yao, bali utakamatwa kwa mkono wa mfalme wa Babeli, nawe utakuwa sababu ya kuteketezwa mji huu.

24Ndipo Sedekia akamwambia Yeremia, Mtu ye yote asipate habari ya maneno haya, nawe hutakufa.

25Lakini kama wakuu wakisikia ya kuwa nimenena nawe, nao wakija kwako, na kukuambia, Tufunulie sasa uliyomwambia mfalme; usimfiche, nasi hatutakuua; na pia uliyoambiwa na mfalme;

26basi, utawaambia, Nalimwomba mfalme asinirudishe nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafa humo.

27Ndipo wakuu wakamwendea Yeremia, wakamwuliza; naye akawaambia sawasawa na maneno aliyoamriwa na mfalme. Basi wakaacha kunena naye; maana neno lile halikujulikana.

28Basi Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi hata siku ile Yerusalemu ulipotwaliwa.