Yeremia - Sura ya 4

Yeremia - Sura ya 4

1Kama ukitaka kurudi, Ee Israeli, asema Bwana, utanirudia mimi; na kama ukitaka kuyaondoa machukizo yako, yasiwe mbele ya macho yangu, ndipo hutaondolewa;

2nawe utaapa hivi, Kama Bwana aishivyo, katika kweli, na katika hukumu, na katika haki ndipo mataifa watajibariki katika yeye, nao watajitukuza katika yeye.

3Maana Bwana awaambia hivi watu wa Yuda na Yerusalemu Ulimeni udongo katika konde zenu, wala msipande mbegu kati ya miiba.

4Jitahirini kwa Bwana, mkaziondoe govi za mioyo yenu, enyi watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikawaka hata mtu asiweze kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.

5Tangazeni katika Yuda, hubirini katika Yerusalemu, na kusema, Pigeni baragumu katika nchi, pigeni kelele sana, na kusema, Jikusanyeni pamoja, tukaingie katika miji yenye boma.

6Twekeni bendera kuelekea Sayuni; kimbieni mpate kuwa salama, msikawie; kwa maana nitaleta mabaya toka kaskazini, na maangamivu makuu.

7Simba ametoka katika kichaka chake, ndiye aangamizaye mataifa; ameanza kushika njia, ametoka katika mahali pake; ili aifanye nchi yako kuwa ukiwa, miji yako ifanywe maganjo, asibaki mwenyeji ndani yake.

8Kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya Bwana haikugeuka na kutuacha.

9Na katika siku hiyo itakuwa, asema Bwana, moyo wa mfalme utapotea, na moyo wa wakuu wake; na makuhani watastaajabu, na manabii watashangaa.

10Nami nikasema, Aa, Bwana MUNGU! Hakika umewadanganya sana watu hawa na Yerusalemu, ukisema, Mtakuwa na amani lakini upanga umeingia katika nafsi za watu.

11Wakati ule watu hawa na Yerusalemu wataambiwa neno hili, Upepo wa moto utokao katika vilele vya nyikani visivyo na miti, ukimwelekea binti ya watu wangu, hauwi upepo wa kupepeta, wala upepo wa kutakasa;

12ni upepo wa nguvu kuliko hizo utakaokuja kwa ajili yangu; sasa mimi nitatoa hukumu juu yao.

13Tazama atapanda juu kama mawingu, na magari yake ya vita yatakuwa kama kisulisuli; farasi zake ni wepesi kuliko tai. Ole wetu, kwa sababu tumeharibika.

14Ee Yerusalemu, jioshe moyo wako usiwe na uovu, upate kuokoka. Mawazo yako mabaya yatakaa ndani yako hata lini?

15Maana sauti yatangaza habari toka Dani, yahubiri uovu toka vilima vya Efraimu;

16Wapasheni mataifa habari; angalieni, hubirini juu ya Yerusalemu, ya kwamba walinzi wanatoka katika nchi ya mbali, wanatoa sauti yao juu ya miji ya Yuda.

17Kama watu walindao shamba, wameuzunguka wauhusuru; kwa sababu ameniasi mimi, asema Bwana.

18Njia yako na matendo yako yamekupatia haya; huu ndio uovu wako; kwa maana ni uchungu, hakika unafikilia hata moyo wako.

19Mtima wangu, mtima wangu! Naumwa katika moyo wangu wa ndani; moyo wangu umefadhaika ndani yangu; siwezi kunyamaza; kwa sababu umesikia, Ee nafsi yangu, sauti ya tarumbeta, mshindo wa vita.

20Uangamivu baada ya uangamivu umetangazwa; kwa maana nchi yote imeharibika; hema zangu zimetekwa nyara ghafula, na mapazia yangu katika dakika moja.

21Niione bendera hata lini, na kuisikia sauti ya tarumbeta?

22Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa.

23Naliiangalia nchi, na tazama, ilikuwa ukiwa, haina watu; naliziangalia mbingu, nazo zilikuwa hazina nuru.

24Naliiangalia milima, na tazama, ilitetemeka, na milima yote ilisogea huko na huko.

25Nikaangalia, na tazama, hapakuwa na mtu hata mmoja, na ndege wote wa angani wamekwenda zao.

26Nikaangalia, na tazama, shamba lililozaa sana limekuwa ukiwa, na miji yake yote ilikuwa imebomoka mbele za Bwana, na mbele za hasira yake kali.

27Maana Bwana asema hivi, Nchi yote itakuwa ukiwa; lakini sitaikomesha kabisa.

28Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na mbingu zitakuwa nyeusi; kwa sababu mimi nimeyanena haya, na kuyakusudia, wala sikujuta wala mimi sitarudi nyuma niyaache.

29Mji mzima unakimbia, kwa sababu ya mshindo wa wapanda farasi na wenye pinde wanaingia vichakani, wanapanda juu ya majabali; kila mji umeachwa, hapana hata mtu mmoja akaaye ndani yake.

30Na wewe, utakapotekwa, utafanyaje? Ujapojivika mavazi mekundu, ujapojipamba mapambo ya dhahabu, ujapojitia wanja machoni, unajifanya kuwa mzuri bure tu; wapenzi wako wanakudharau; wanakutafuta roho yako.

31Kwa maana nimesikia sauti, kama sauti ya mwanamke wakati wa utungu wake, na sauti yake aumwaye, kama mwanamke azaaye mtoto wake wa kwanza, sauti ya binti Sayuni, atwetaye kupata pumzi, na kunyosha mikono yake, akisema, Ole wangu, sasa! Kwa maana roho yangu inazimia mbele ya wauaji.