Yeremia - Sura ya 40

Yeremia - Sura ya 40

1Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, baada ya wakati ule Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, alipomwacha aende zake toka Rama, baada ya kumchukua hali ya kufungwa minyororo, pamoja na wafungwa wote wa Yerusalemu na Yuda, waliochukuliwa hali ya kufungwa mpaka Babeli.

2Naye amiri wa askari walinzi akamtwaa Yeremia, akamwambia, Bwana, Mungu wako, alitamka mabaya haya juu ya mahali hapa;

3naye Bwana ameyaleta, na kufanya kama alivyosema; kwa sababu mmemwasi Bwana, wala hamkuitii sauti yake; ndiyo maana neno hili limewajia ninyi.

4Na sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama ukiona ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana; lakini kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama, nchi yote i mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, enenda huko.

5Alipokuwa bado hajaenda, akasema, Rudi sasa kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa liwali juu ya miji ya Yuda, ukakae pamoja naye kati ya watu; au enenda po pote utakapoona mwenyewe kuwa pakufaa. Basi, amiri wa askari walinzi akampa vyakula na zawadi, akamwacha aende zake.

6Basi, Yeremia akaenda kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, huko Mizpa, akakaa pamoja naye kati ya watu wale waliosalia katika nchi.

7Kisha, wakuu wote wa majeshi waliokuwa katika bara, wao na watu wao, waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemweka Gedalia, mwana wa Ahikamu, kuwa liwali juu ya nchi, na kwamba amemkabidhi wanaume na wanawake na watoto, na baadhi ya maskini wa nchi wasiochukuliwa mateka Babeli;

8ndipo wakamwendea Gedalia huko Mizpa; nao ni hawa, Ishmaeli, mwana wa Nethania, na Yohana na Yonathani, wana wa Karea, na Seraya, mwana wa Tanhumethi, na wana wa Efai, Mnetofa, na Yezania, mwana wa Mmaaka, wao na watu wao.

9Na Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, akawaapia wao na watu wao, akisema, Msiogope kuwatumikia Wakaldayo; kaeni katika nchi, mkamtumikie mfalme wa Babeli; nayo itawafaa.

10Na mimi, tazama, nitakaa Mizpa, ili nisimame mbele ya Wakaldayo watakaotujilia; lakini ninyi chumeni divai, na matunda ya wakati wa jua, na mafuta, mkaviweke vitu hivyo katika vyombo vyenu, mkakae katika miji yenu mliyoitwaa.

11Kadhalika waliposikia Wayahudi wote, waliokuwa katika Moabu, na kati ya wana wa Amoni, na hao waliokuwa katika Edomu, na hao waliokuwa katika nchi zote, ya kuwa mfalme wa Babeli amewaachia Yuda mabaki, na ya kuwa amemweka Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, juu yao;

12basi, Wayahudi wote wakarudi kutoka kila mahali walikofukuzwa wakaenda mpaka nchi ya Yuda, wakamwendea Gedalia huko Mizpa, wakakusanya divai, na matunda ya wakati wa jua mengi sana.

13Tena Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi ya barani, wakamwendea Gedalia huko Mizpa,

14wakamwambia, Je! Una habari wewe ya kuwa Baalisi, mfalme wa wana wa Amoni, amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania, akuue? Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, hakusadiki neno hili.

15Basi, Yohana, mwana wa Karea, akamwambia Gedalia huko Mizpa kwa siri, akisema, Niache niende nikampige Ishmaeli, mwana wa Nethania, wala hapana mtu atakayejua jambo hili; kwani akuue wewe, hata wakatawanyike Wayahudi waliokukusanyikia, na mabaki ya Yuda wakaangamie?

16Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, akamwambia Yohana, mwana wa Karea, Usilitende jambo hili, maana unamsingizia Ishmaeli.