Yeremia - Sura ya 49

Yeremia - Sura ya 49

1Habari za wana wa Amoni. Bwana asema hivi, Je, Israeli hana wana? Je! Hana mrithi? Basi, mbona Malkamu anamiliki Gadi, na watu wake wanakaa katika miji yake?

2Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakaposikizisha mshindo wa vita juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema Bwana.

3Piga yowe, Ee Heshboni, Kwa maana Ai umeangamizwa; Lieni, enyi binti za Raba, Mjivike nguo za magunia; Ombolezeni, mkipiga mbio Huko na huko kati ya maboma; Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa, Makuhani wake na wakuu wake pamoja.

4Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijilia?

5Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, Bwana wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao.

6Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema Bwana.

7Habari za Edomu. Bwana wa majeshi asema hivi, Je! Hapana tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao?

8Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia.

9Je! Kama wachuma zabibu wangekujia, wasingeacha zabibu ziokotwe? Kama wangekujia wevi usiku, wasingeharibu hata watakapopata vya kutosha?

10Lakini nimemwacha Esau hana kitu, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko.

11Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi.

12Maana Bwana asema hivi, Tazama, wale wasioandikiwa kunywea kikombe, watakinywea, ni hakika; na wewe je! U mtu ambaye hataadhibiwa kabisa? Hukosi utaadhibiwa, naam, kunywa utakunywa.

13Kwa maana nimeapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, kwamba Bozra utakuwa ajabu, na aibu, na ukiwa, na laana; na miji yake yote itakuwa ukiwa wa daima.

14Nimepata habari kwa Bwana, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Jikusanyeni, mkaujie, Mkainuke kwenda vitani.

15Maana nimekufanya mdogo kati ya mataifa, Na kudharauliwa katika watu.

16Katika habari za kuogofya kwako, Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Ushikaye kilele cha milima; Ujapofanya kioto chako juu sana kama tai, Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana.

17Na Edomu atakuwa ajabu; kila mtu apitaye atashangaa, na kuzomea, kwa sababu ya mapigo yake yote.

18Kama vile vilivyotokea wakati wa kuangushwa Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema Bwana; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.

19Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?

20Basi, lisikieni shauri la Bwana; Alilolifanya juu ya Edomu; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu yao wakaao Temani; Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao.

21Nchi yatetemeka kwa sauti ya kuanguka kwao; Kuna kilio, sauti yake yasikiwa katika Bahari ya Shamu.

22Tazama, atapanda na kuruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Bozra; na mioyo ya mashujaa wa Edomu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wake.

23Habari za Dameski. Hamathi umetahayarika, na Arpadi pia; Maana wamesikia habari mbaya; Wameyeyuka kabisa; Huzuni iko baharini, haiwezi kutulia.

24Dameski umedhoofika; Umejigeuza kukimbia; tetemko limeushika; Dhiki na huzuni zimeupata, Kama za mwanamke katika utungu wake.

25Imekuwaje mji wa sifa haukuachwa, mji wa furaha yangu?

26Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wote wa vita watanyamazishwa katika siku hiyo, asema Bwana wa majeshi.

27Nami nitawasha moto katika ukuta wa Dameski, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.

28Habari za Kedari, na za falme za Hazori, ambazo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alizipiga. Bwana asema hivi, Ondokeni, pandeni hata Kedari, mkawateke nyara wana wa mashariki.

29Hema zao na makundi yao watayatwaa; watachukulia mbali mapazia yao kwa faida yao wenyewe, na vyombo vyao vyote, na ngamia zao; nao watawapigia kelele wakisema, Hofu ziko pande zote.

30Kimbieni ninyi, enendeni mbali mkitanga-tanga, kaeni chini sana, enyi mkaao Hazori, asema Bwana; maana Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amefanya shauri juu yenu, naye amekusudia neno juu yenu.

31Ondokeni, pandeni hata taifa lililo katika hali ya raha, likaalo bila kuhangaika, asema Bwana; wasio na malango wala makomeo, wakaao peke yao.

32Na ngamia zao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya hata pepo zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema Bwana.

33Na Hazori utakuwa kao la mbwa-mwitu; ukiwa milele; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.

34Neno la Bwana lililomjia Yeremia, nabii, juu ya Elamu, mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, kusema,

35Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama nitauvunja upinde wa Elamu, ulio mkuu katika nguvu zao.

36Na juu ya Elamu nitazileta pepo nne, toka pembe nne za mbinguni, nami nitawatawanya hata pepo nne zote, wala hapana taifa ambalo hawatalifikilia watu wa Elamu waliofukuzwa.

37Nami nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya adui zao, na mbele ya hao wanaowatafuta roho zao; nami nitawaletea mabaya, naam, hasira yangu kali, asema Bwana; nami nitautuma upanga uwafuatie, hata nitakapowaangamiza;

38nami nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu, nami nitawaharibu, mfalme na wakuu, watoke huko, asema Bwana.

39Lakini itakuwa, katika siku za mwisho, nitawarudisha wafungwa wa Elamu, asema Bwana.