Yeremia - Sura ya 7

Yeremia - Sura ya 7

1Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,

2Simama langoni pa nyumba ya Bwana, ukatangaze hapo neno hili, ukisema, Sikilizeni neno la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mnaoingia katika malango haya ili kumwabudu Bwana.

3Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa.

4Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya.

5Maana kama mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu; kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake;

6kama hamwonei mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe;

7ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele.

8Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia.

9Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua;

10kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote?

11Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang'anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana.

12Lakini enendeni sasa hata mahali pangu palipokuwapo katika Shilo, nilipolikalisha jina langu hapo kwanza, mkaone nilivyopatenda kwa sababu ya uovu wa watu wangu Israeli.

13Na sasa, kwa sababu mmezifanya kazi hizi zote asema Bwana, nami nikasema nanyi, nikiamka mapema na kunena, lakini hamkusikia; nami nikawaita wala hamkuniitikia;

14basi, nitaitenda nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, mnayoitumainia, na mahali hapa nilipowapa ninyi na baba zenu, kama nilivyopatenda Shilo.

15Nami nitawatupa ninyi mbali na macho yangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote, yaani, wazao wote wa Efraimu.

16Basi, wewe usiwaombee watu hawa, wala usiwapazie sauti yako, wala kuwaombea dua, wala usinisihi kwa ajili yao; kwa maana sitakusikiliza.

17Je! Huoni wanavyotenda katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu?

18Watoto huokota kuni, na baba zao huwasha moto, na wanawake hukanda unga, ili kumfanyizia mikate malkia wa mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kinywaji, wapate kunikasirisha mimi.

19Je! Watu hawa wanikasirisha mimi? Asema Bwana; hawajikasirishi nafsi zao, na kuzitia haya nyuso zao wenyewe?

20Kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, hasira yangu na ghadhabu yangu zitamwagwa juu ya mahali hapa, juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya miti ya mashamba, na juu ya mazao ya nchi; nayo itateketea, isizimike.

21Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tieni sadaka zenu za kuteketezwa pamoja na dhabihu zenu, mkale nyama.

22Maana sikusema na baba zenu, wala sikuwaamuru kwa habari za sadaka za kuteketezwa na dhabihu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri;

23lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa.

24Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele.

25Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku, na kuwatuma.

26Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao.

27Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza, nawe utawaita; lakini hawatakuitikia.

28Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao.

29Zikate nywele zako, Ee Yerusalemu, uzitupe, Ukafanye maombolezo juu ya vilele vya milima; Kwa maana Bwana amekikataa na kukitupa Kizazi cha ghadhabu yake.

30Maana wana wa Yuda wametenda yaliyo maovu machoni pangu, asema Bwana; wameweka machukizo yao ndani ya nyumba hiyo, iitwayo kwa jina langu, hata kuitia unajisi.

31Nao wamepajenga mahali palipoinuka pa Tofethi, palipo katika bonde la mwana wa Hinomu, ili kuwateketeza wana wao na binti zao motoni; jambo ambalo mimi sikuliagiza, wala halikuingia moyoni mwangu.

32Basi angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo katika siku hizo halitaitwa tena Tofethi, wala Bonde la mwana wa Hinomu bali litaitwa, Bonde la Machinjo; maana watazika watu katika Tofethi, hata hapatakuwapo mahali pa kuzika tena.

33Na mizoga ya watu hawa itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi; wala hapana mtu atakayewafukuza.

34Ndipo katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, nitaikomesha sauti ya kicheko na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi na sauti ya bibi arusi; kwa maana nchi hiyo itakuwa ukiwa.