Ayubu - Sura ya 10

Ayubu - Sura ya 10

1Nafsi yangu inachoka na maisha yangu; Sitajizuia na kuugua kwangu; Nitanena kwa uchungu wa roho yangu.

2Nitamwambia Mungu, Usinihukumie makosa; Nionyeshe sababu ya wewe kushindana nami.

3Je! Ni vema kwako wewe kuonea, Na kuidharau kazi ya mikono yako, Na kuyaangazia mashauri ya waovu?

4Je! Wewe una macho ya kimwili, Au je! Waona kama aonavyo binadamu?

5Je! Siku zako ni kama siku za mtu, Au je! Miaka yako ni kama siku za mtu,

6Hata ukauliza-uliza habari za uovu wangu, Na kuitafuta dhambi yangu,

7Ujapojua ya kuwa mimi si mwovu; Wala hapana awezaye kuokoa na mkono wako?

8Mikono yako imeniumba na kunifinyanga; Nawe utageuka na kuniangamiza?

9Kumbuka, nakusihi ulivyonifinyanga kama vile udongo; Nawe, je! Utanirudisha uvumbini tena?

10Je! Wewe hukunimimina kama maziwa, Na kunigandisha mfano wa jibini?

11Umenivika ngozi na nyama, Na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa.

12Umenijazi uhai na upendeleo, Na maangalizi yako yameilinda roho yangu.

13Lakini mambo haya uliyaficha moyoni mwako; Najua kuwa haya yamo nafsini mwako;

14Nikifanya dhambi, ndipo waniangalia, Wala hutaniachilia na uovu wangu.

15Mimi nikiwa mbaya, ole wangu! Nami nikiwa mwenye haki, walakini sitainua kichwa changu; Mimi nimejaa aibu Na kuyaangalia mateso yangu.

16Kichwa changu kikijiinua, waniwinda kama simba; Tena wajionyesha kwangu kuwa wa ajabu.

17Wewe warejeza upya hao mashahidi yako juu yangu, Na kasirani yako waiongeza juu yangu; Jeshi kwa jeshi juu yangu.

18Kwa nini basi kunitoa tumboni? Ningekata roho, lisinione jicho lo lote.

19Ningalikuwa kama mtu asiyekuwapo; Ningalichukuliwa kaburini kutoka tumboni.

20Je! Siku zangu si chache? Acha basi, Usinisumbue, nipate ngaa kutuzwa moyo kidogo.

21Kabla sijaenda huko ambako sitarudi kutoka huko tena, Ni hiyo nchi ya giza, giza tupu;

22Ni nchi ya giza kuu, kama giza lenyewe lilivyo; Ni nchi ya giza tupu, isiyo na matengezo ya mambo yo yote, Nchi ambayo nuru yake ni kama giza.