Ayubu - Sura ya 11

Ayubu - Sura ya 11

1Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu, na kusema,

2Je! Huu wingi wa maneno usijibiwe? Na mtu aliyejaa maneno, je! Ahesabiwe kuwa na haki?

3Je! Majivuno yako yawanyamazishe watu wawe kimya? Nawe hapo ufanyapo dhihaka, je! Hapana mtu atakayekutahayarisha?

4Kwa kuwa wewe wasema, Mafunzo yangu ni safi, Nami ni safi machoni pako.

5Lakini, laiti Mungu angenena, Na kuifunua midomo yake juu yako;

6Tena akuonyeshe hizo siri za hekima, Ya kuwa hufanikiwa katika kuyatimiza makusudi yake! Ujue basi ya kuwa Mungu akuachilia katika uovu wako.

7Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu? Waweza kuufikilia upeo wa huyo Mwenyezi?

8Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe?

9Cheo chake ni kirefu kuliko dunia, Ni kipana zaidi ya bahari.

10Yeye akipita, na kufunga watu, Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia?

11Kwani yeye awajua watu baradhuli; Huona na uovu pia, hata asipoufikiri.

12Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu, Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda-mwitu.

13Wewe ukiuweka moyo wako kwa uelekevu, Na kumnyoshea mikono yako;

14Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe, Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako;

15Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila; Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu;

16Kwa kuwa utasahau mashaka yako; Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita;

17Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri; Lijapokuwa ni giza, litakuwa kama alfajiri.

18Nawe utakuwa salama, kwa sababu kuna matumaini; Naam, utatafuta-tafuta kando yako, na kupumzika katika salama.

19Tena utalala, wala hapana atakayekutia hofu; Naam, wengi watakutafuta uso wako.

20Lakini macho ya waovu yataingia kiwi, Nao hawatakuwa na njia ya kukimbilia, Na matumaini yao yatakuwa ni kutoa roho.