Ayubu - Sura ya 17

Ayubu - Sura ya 17

1Roho yangu imezimika, siku zangu zimekoma, Kaburi i tayari kunipokea.

2Ni kweli wako kwangu wenye kufanya dhihaka, Jicho langu hukaa katika kunifanyia uchungu kwao.

3Nipe rehani basi, uwe dhamana kwa ajili yangu kwako wewe mwenyewe; Kuna nani atakayeniwekea dhamana?

4Kwani mioyo yao imeificha ufahamu; Kwa hiyo hutawakuza.

5Awafitiniye rafiki zake wawe mawindo, Hata macho ya watoto wake yataingia kiwi.

6Amenifanya niwe simo kwa watu; Nimekuwa mwenye kuchukiwa kwa wazi.

7Jicho langu nalo limekuwa giza kwa sababu ya majonzi, Na via vyangu vyote vimekuwa kama kivuli.

8Walekevu watayastaajabia hayo, Na asiye na hatia atajiamsha juu ya mpotovu.

9Lakini mwenye haki ataishika njia yake, Naye mwenye mikono safi atazidi kupata nguvu.

10Lakini rudini; ninyi nyote, njoni sasa; Wala sitampata mtu mwenye hekima kati yenu.

11Siku zangu zimepita, makusudi yangu yamevunjika, Hata hayo niliyo nayo moyoni mwangu.

12Wabadili usiku kuwa mchana; Wasema, Mwanga u karibu kwa sababu ya giza.

13Nikitazamia kuzimu kuwa nyumba yangu; Nikitandika malazi yangu gizani;

14Ikiwa nimeuita uharibifu, Wewe u baba yangu; Na kuliambia buu, Wewe u mama yangu, na umbu langu;

15Basi, tumaini langu li wapi? Na tumaini langu, ni nani atakayeliona?

16Litashuka kwenye makomeo ya kuzimu, Itakapokuwapo raha mavumbini.