Ayubu - Sura ya 18

Ayubu - Sura ya 18

1Ndipo Bildadi, Mshuhi, akajibu, na kusema,

2Je! Hata lini utayategea maneno mitambo? Fikiri, kisha baadaye tutanena.

3Twahesabiwa kuwa wanyama kwa sababu gani, Tena kuwa wanajisi machoni pako?

4Wewe ujiraruaye mwenyewe katika hasira yako, Je! Dunia itaachwa kwa ajili yako wewe? Au jabali litaondolewa mahali pake?

5Naam, mwanga wa waovu utazimika, Wala mwali wa moto wake hautang'aa.

6Mwanga hemani mwake utakuwa giza, Nayo taa iliyo juu yake itazimishwa.

7Hatua zake za nguvu zitasongwa, Na shauri lake mwenyewe litamwangusha chini.

8Kwani ametupwa katika wavu na miguu yake mwenyewe, Naye huenda juu ya matanzi.

9Tanzi litamshika kisigino chake, Na mtambo utamgwia.

10Amefichiwa tanzi chini, Na mtego amewekewa njiani.

11Matisho yatamtia hofu pande zote, Na kumfukuza karibu na visigino vyake.

12Nguvu zake zitaliwa na njaa, Na msiba utakuwa tayari kwa kusita kwake.

13Utakula via vya mwili wake, Naam, mzaliwa wa kwanza wa mauti atavila via vyake.

14Atang'olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini; Naye atapelekwa kwake mfalme wa utisho.

15Ambacho si chake kitakaa katika hema yake; Kiberiti kitamwagwa juu ya makazi yake.

16Chini, mizizi yake itakaushwa; Na juu, tawi lake litasinyaa.

17Kumbukumbu lake litakoma katika nchi, Wala hatakuwa na jina mashambani.

18Atakimbizwa kutoka mwangani hata gizani, Na kufukuzwa atoke duniani.

19Hatakuwa na mwana wala mjukuu kati ya watu wake, Wala hatasalia mtu hapo alipokaa.

20Hao wanaokaa magharibi watastaajabia siku yake, Kama vile wanaokaa mashariki walivyotiwa hofu.

21Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotovu, Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu.