Ayubu - Sura ya 21

Ayubu - Sura ya 21

1Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2Yasikizeni sana maneno yangu; Jambo hili na liwe faraja yenu.

3Niacheni, nami pia nitanena; Tena nikiisha nena, zidini kudhihaki.

4Mimi, je! Mashitaka yangu yamhusu mwanadamu? Nami kwa nini nisikose kusubiri?

5Niangalieni, mkastaajabu, Mkaweke mkono kinywani.

6Hata nikumbukapo nahuzunika, Na utisho wanishika mwilini mwangu.

7Mbona waovu wanaishi, Na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu?

8Kizazi chao kinathibitika nao machoni pao, Na wazao wao mbele ya macho yao.

9Nyumba zao zi salama pasina hofu, Wala fimbo ya Mungu haiwapigi.

10Fahali wao huvyaza wala hapungukiwi na nguvu; Ng'ombe wao mke huzaa, asiharibu mimba.

11Huwatoa kama kundi watoto wao. Na watoto wao hucheza.

12Huimba kwa matari na kwa kinubi, Na kuifurahia sauti ya filimbi.

13Siku zao hutumia katika kufanikiwa, Kisha hushuka kuzimuni ghafula.

14Walakini walimwambia Mungu. Tuondokee; Kwani hatutaki kuzijua njia zako.

15Huyo Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie? Nasi tutafaidiwa nini tukimwomba?

16Tazama, kufanikiwa kwao hakumo mkononi mwao; Mashauri ya waovu na yawe mbali nami.

17Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimishwa? Na msiba wao kuwajilia? Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake?

18Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo, Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba?

19Mwasema, Mungu huwawekea watoto wa mtu huo uovu wake. Na amlipe mwenyewe, ili apate kuujua.

20Macho yake mwenyewe na yaone uharibifu wake, Akanywe ghadhabu zake Mwenyezi.

21Kwani ana furaha gani katika mbari yake baada yake, Hesabu ya miezi yake itakapokwisha katwa katikati?

22Je! Mtu awaye yote atamfundisha Mungu maarifa? Naye ndiye awahukumuye walioko juu.

23Mmoja hufa katika nguvu zake kamili, Mwenye kukaa salama na kustarehe;

24Vyombo vyake vimejaa maziwa, Na mafuta ya mifupani mwake ni laini.

25Mwingine hufa katika uchungu wa roho, Asionje mema kamwe.

26Wao hulala mavumbini sawasawa, Mabuu huwafunika.

27Tazama, nayajua mawazo yenu, Na mashauri mnayoazimia kwa uovu juu yangu.

28Kwa kuwa mwasema, Nyumba ya huyo mkuu i wapi? Na hema waliyoikaa hao waovu i wapi?

29Je! Hamkuwauliza wapitao njiani? Na maonyo yao hamyajui?

30Kwamba mwovu huachiliwa katika siku ya msiba? Na kuongozwa nje katika siku ya ghadhabu?

31Ni nani atakayetangaza njia yake usoni pake? Tena ni nani atakayemlipa kwa hayo aliyofanya?

32Pamoja na hayo atachukuliwa kaburini, Nao watalinda zamu juu ya ziara lake.

33Udongo wa bondeni utakuwa tamu kwake, Na watu wote watafuata nyuma yake, Kama vile walivyomtangulia watu wasiohesabika.

34Basi imekuwaje ninyi kunituza moyo bure, Kwa kuwa katika jawabu zenu unasalia uongo tu.