Ayubu - Sura ya 22

Ayubu - Sura ya 22

1Ndipo huyo Elifazi Mtemani akajibu, na kusema,

2Je! Yumkini mtu awaye yote kumfaa Mungu? Hakika yeye aliye na hekima hujifaa mwenyewe.

3Je! Mwenyezi hupata furaha katika wewe kuwa mwenye haki? Au je, ni faida kwake, kwamba wafanya njia zako kuwa timilifu?

4Je! Ni kwa wewe kumcha yeye anakukemea? Na kuingia hukumuni nawe?

5Je! Uovu wako si mkuu? Wala maovu yako hayana mwisho.

6Kwa kuwa umetwaa dhamana kwa nduguyo bure, Na kuwavua nguo zao walio uchi.

7Hukumpa maji ya kunywa huyo aliyechoka, Nawe umemnyima chakula huyo mwenye njaa.

8Lakini huyo shujaa, nchi ilikuwa yake; Na huyo mwenye kusifiwa, yeye aliikaa.

9Umewafukuza wanawake wajane hali ya utupu, Na mikono ya mayatima imevunjwa.

10Kwa hiyo umezungukwa na mitego, Na hofu ya ghafula yakutaabisha,

11Au je! Huoni giza, Na maji mengi yanayokufunika?

12Je! Mungu hayuko mbinguni juu? Tena tazama umbali wa nyota, jinsi zilivyo juu!

13Nawe wasema, Mungu anajua nini? Je! Aweza kuamua kati ya giza kuu?

14Mawingu mazito ni kifuniko chake, hata asione; Naye yuatembea juu ya kuba ya mbingu.

15Je! Utaiandama njia ya zamani Waliyoikanyaga watu waovu?

16Ambao walinyakuliwa kabla ya wakati wao, Msingi wao ulimwagika kama kijito cha maji;

17Waliomwambia Mungu, Tuondokee; Tena, Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?

18Naye ndiye aliyezijaza nyumba zao vitu vyema; Lakini mashauri ya waovu na yawe mbali nami.

19Wenye haki huyaona hayo wakafurahi; Nao wasio na hatia huwacheka;

20Wasema, Hakika hao waliotuinukia wamekatiliwa mbali, Na mabaki yao moto umeyateketeza.

21Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.

22Uyapokee, tafadhali, mafunzo yatokayo kinywani mwake, Na maneno yake yaweke moyoni mwako.

23Ukimrudia Mwenyezi, utajengwa; Ukiuondoa udhalimu mbali na hema yako.

24Nawe hazina zako ziweke mchangani, Na dhahabu ya Ofiri iweke kati ya mawe ya vijito;

25Naye Mwenyezi atakuwa hazina yako, Atakuwa ni fedha ya thamani kwako.

26Kwani ndipo utakapojifurahisha katika Mwenyezi, Na kuinua uso wako kumwelekea Mungu.

27Utamwomba yeye naye atakusikia; Nawe utazitimiliza nadhiri zako.

28Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako.

29Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.

30Atamwokoa na huyo asiye na hatia; Naam, utaokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.