Ayubu - Sura ya 23

Ayubu - Sura ya 23

1Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2Hata leo mashitaka yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.

3Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa!

4Ningeiweka daawa yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja.

5Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa na hayo atakayoniambia.

6Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza.

7Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele.

8Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona;

9Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone.

10Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.

11Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.

12Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,

13Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza? Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo.

14Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamuriwa; Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye.

15Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake; Nitakapofikiri, namwogopa.

16Kwani Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia, Naye Mwenyezi amenitaabisha;

17Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza, Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.