Ayubu - Sura ya 26

Ayubu - Sura ya 26

1Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2Jinsi ulivyomsaidia huyo asiye na uwezo! Jinsi ulivyouokoa mkono usio na nguvu!

3Jinsi ulivyomshauri huyo asiye na hekima! Na kutangaza ujuzi wa kweli kwa wingi!

4Je! Umetamka maneno kwa nani? Kisha ni roho ya nani iliyotoka kwako?

5Hao waliokufa watetema Chini ya maji na hao wayakaao.

6Kaburi li wazi mbele yake, Uharibifu nao hauna kifuniko.

7Yeye hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, Na kuutundika ulimwengu pasipo kitu.

8Huyafunga maji ndani ya mawingu yake mazito; Na hilo wingu halipasuki chini yake.

9Husitiri uso wa kiti chake cha enzi, Na kulitandaza wingu lake juu yake.

10Amepiga duara kuwa ni mpaka juu ya uso wa maji, Hata hapo mwanga na giza vinapopakana.

11Nguzo za mbingu zatetemeka, Na kustaajabu kwa kukemea kwake.

12Huichafua bahari kwa uwezo wake, Na kumtema Rahabu kwa akili zake.

13Hizo mbingu hupambwa kwa roho yake; Mkono wake umemchoma nyoka aendaye mbio.

14Tazama, hivi ni viunga tu vya njia zake; Na jinsi yalivyo madogo manong'ono tusikiayo katika habari zake! Lakini ngurumo za uweza wake ni nani awezaye kuelewa nazo?