Ayubu - Sura ya 27

Ayubu - Sura ya 27

1Kisha Ayubu akaendelea na mithali yake, na kusema,

2Kama aishivyo Mungu, aliyeniondolea haki yangu; Huyo Mwenyezi aliyeitesa nafsi yangu;

3(Kwa kuwa uhai wangu ukali mzima ndani yangu, Na roho ya Mungu i katika pua yangu;)

4Hakika midomo yangu haitanena yasiyo haki, Wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.

5Hasha! Nisiwahesabie ninyi kuwa na haki; Hata nitakapokufa sitajiondolea uelekevu wangu.

6Haki yangu naishika sana, wala sitaiacha; Moyo wangu hautanisuta wakati nikiwapo hai.

7Adui yangu na awe kama huyo mwovu, Na mwenye kuondoka kinyume changu na awe kama asiye haki.

8Kwani tumaini la mpotovu ni nini, ingawa ajipatia faida, Hapo Mungu amwondoleapo roho yake?

9Je! Mungu atakisikia kilio chake, Taabu zitakapomfikilia?

10Je! Atajifurahisha katika Mwenyezi, Na kumlingana Mungu nyakati zote?

11Nitawafundisha ninyi mambo ya mkono wa Mungu; Hayo yaliyo kwa Mwenyezi sitayaficha.

12Tazama, ninyi nyote mmeyaona wenyewe; Mbona basi mmebatilika kabisa?

13Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu kwa Mungu, Na urithi wa hao waoneao, waupokeao kwa Mwenyezi.

14Watoto wake wakiongezeka ni kwa upanga; Na wazao wake hawatashiba chakula.

15Hao watakaosalia kwake watazikwa katika kufa, Wala wajane wake waliofiwa na waume hawataomboleza.

16Ajapokusanya fedha kama mavumbi, Na kujifanyia mavazi kama udongo kwa wingi;

17Yumkini kuyatengeza, lakini wenye haki watayavaa, Nao wasio na hatia watazigawanya hizo fedha.

18Yeye hujenga nyumba yake kama mdudu, Na kama kibanda afanyacho mlinzi.

19Yeye hujilaza hali ni tajiri, lakini ndio mwisho; Hufunua macho yake, naye hayuko.

20Vitisho vyampata kama maji mengi; Dhoruba humwiba usiku.

21Upepo wa mashariki humchukua, naye huondoka; Na kumkumba atoke mahali pake.

22Kwani Mungu atamtupia asimhurumie; Angependa kuukimbia mkono wake.

23Watu watampigia makofi, Na kumzomea atoke mahali pake.