Ayubu - Sura ya 29

1Kisha Ayubu akaendelea na mithali yake, na kusema,
2Laiti ningekuwa kama nilivyokuwa katika miezi ya kale, Kama katika siku hizo Mungu aliponilinda;
3Hapo taa yake ilipomulika juu yangu kichwani, Nami nilitembea gizani kwa njia ya mwanga wake;
4Kama nilivyokuwa katika siku zangu za kukomaa, Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu;
5Wakati Mwenyezi alipokuwa akali pamoja nami, Nao watoto wangu walipokuwa wakinizunguka;
6Wakati hatua zangu zilipokuwa zikioshwa kwa siagi, Nalo jabali liliponimiminia mito ya mafuta!
7Wakati nilipotoka kwenda mjini, hata langoni, Nilipokitengeza kiti changu katika njia kuu,
8Hao vijana waliniona wakajificha, Nao wazee wakaniondokea na kusimama;
9Wakuu wakanyamaa wasinene, Na kuweka mikono yao vinywani mwao;
10Sauti yao masheki ilinyamaa, Na ndimi zao zilishikamana na makaakaa yao.
11Maana sikio liliponisikia, ndipo likanibarikia; Na jicho liliponiona, likanishuhudia.
12Kwa sababu nalimwokoa maskini aliyenililia; Yatima naye, na yule asiyekuwa na mtu wa kumsaidia.
13Baraka yake yeye aliyekuwa karibu na kupotea ilinijia; Nikaufanya moyo wa mjane kuimba kwa furaha.
14Nalijivika haki, ikanifunika, Adili yangu ilikuwa kama joho na kilemba.
15Nalikuwa macho kwa kipofu, Nalikuwa miguu kwa aliyechechemea.
16Nalikuwa baba kwa mhitaji, Na daawa ya mtu nisiyemjua naliichunguza.
17Nami nilizivunja taya za wasio haki, Na kumpokonya mawindo katika meno yake.
18Ndipo niliposema, Nitakufa ndani ya kioto changu, Nami nitaziongeza siku zangu kama mchanga;
19Shina langu limeenea hata kufika majini, Na umande hukaa usiku kucha katika matawi yangu;
20Utukufu wangu utakuwa mpya kwangu, Na uta wangu hurejezwa upya mkononi mwangu.
21Watu walitega masikio kunisikiliza, na kungoja, Wakanyamaa kimya wapate sikia mashauri yangu.
22Hawakunena tena baada ya kusikia maneno yangu; Matamko yangu yakadondoka juu yao.
23Walikuwa wakiningojea kama kungojea mvua; Wakafunua vinywa vyao sana kama mvua ya masika.
24Walipokata tamaa nikacheka nao; Na mwanga wa uso wangu hawakuuangusha.
25Niliwachagulia njia, nikakaa kama mkuu wao. Nikakaa kama mfalme katika jeshi la askari, Mfano wa awafarijiye hao waombolezao.