Ayubu - Sura ya 3

Ayubu - Sura ya 3

1Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake.

2Ayubu akajibu, na kusema;

3Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba.

4Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie.

5Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe.

6Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi.

7Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe.

8Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo lewiathani.

9Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone makope ya asubuhi;

10Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni.

11Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni?

12Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya?

13Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika;

14Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni;

15Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza fedha nyumba zao;

16Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa.

17Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wapumzika

18Huko wafungwa waona raha pamoja; Hawaisikii sauti yake msimamizi.

19Wakuu na wadogo wako huko; Mtumishi yu huru kwa bwana wake.

20Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai;

21Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika;

22Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi?

23Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo?

24Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji.

25Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia.

26Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini huja taabu.