Ayubu - Sura ya 31

Ayubu - Sura ya 31

1Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?

2Kwani sehemu ya Mungu itokayo juu ingekuwa nini, Na urithi wa Mwenyezi utokao juu?

3Je! Siyo msiba kwa wasio haki, Na hasara kwao watendao uovu?

4Je! Yeye hazioni njia zangu, Na kuzihesabu hatua zangu zote?

5Kwamba nimetembea katika ubatili, Na mguu wangu umeukimbilia udanganyifu;

6(Na nipimwe katika mizani iliyo sawasawa, Ili Mungu aujue uelekevu wangu);

7Kwamba hatua yangu imekengeuka na kuiacha njia, Na moyo wangu kuyaandama macho yangu, Tena kwamba kipaku cho chote kimeshikamana na mikono yangu;

8Basi na nipande, mwingine ale; Naam, mazao ya shamba langu na yang'olewe.

9Kama moyo wangu ulishawishwa kwa mwanamke, Nami nimeotea mlangoni pa jirani yangu;

10Ndipo hapo mke wangu na asage kwa mwingine, Na wengine na wainame juu yake.

11Kwani hilo lingekuwa kosa kuu; Naam, lingekuwa ni uovu wa kuadhibiwa na waamuzi;

12Kwa kuwa ni moto uteketezao hata Uharibifu, Nao ungeyang'oa maongeo yangu yote.

13Kama nimeidharau daawa ya mtumishi wangu, au ya kijakazi changu, Waliposhindana nami;

14Basi Mungu atakapoinuka nitafanya nini? Naye atakapozuru, nitamjibuje?

15Je! Huyo aliyenifanya mimi ndani ya tumbo, siye aliyemfanya na yeye? Si yeye mmoja aliyetufinyanga tumboni?

16Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, Au kama nimeyatia kiwi macho ya mwanamke mjane;

17Au kama nimekula tonge langu peke yangu, Mayatima wasipate kulila;

18(La, tangu ujana wangu alikua pamoja nami kama kwa baba; Nami nimekuwa ni kiongozi cha mjane tangu tumbo la mamangu);

19Ikiwa nimemwona mtu kuangamia kwa kukosa nguo, Au wahitaji kukosa mavazi;

20Ikiwa viuno vyake havikunibarikia, Au kama hakupata moto kwa manyoya ya kondoo zangu;

21Ikiwa nimewainulia mayatima mkono, Nilipoona msaada wangu langoni;

22Basi bega langu na lianguke kutoka mahali pake, Na mkono wangu uvunjike mfupani mwake.

23Kwani msiba utokao kwa Mungu ulikuwa na kitisho kwangu, Na kwa sababu ya ukuu wake sikuweza kufanya neno.

24Ikiwa nimeifanya dhahabu kuwa tumaini langu, Na kuiambia dhahabu safi, Wewe u tegemeo langu;

25Kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi, Na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi;

26Kama nililitazama jua lilipoangaza, Au mwezi ukiendelea katika kung'aa;

27Na moyo wangu umeshawishwa kwa siri, Na midomo yangu imeubusu mkono wangu;

28Hilo nalo lingekuwa uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; Kwani ningemwambia uongo Mungu aliye juu.

29Kama nilifurahi kwa kuangamia kwake huyo aliyenichukia, Au kujitukuza alipopatikana na maovu;

30(Naam, sikukiacha kinywa changu kufanya dhambi Kwa kuutaka uhai wake kwa kuapiza);

31Kama watu wa hemani mwangu hawakunena, Ni nani awezaye kumpata mtu asiyeshibishwa na yeye kwa nyama?

32Mgeni hakulala njiani; Lakini nilimfungulia msafiri milango yangu;

33Ikiwa kama mwanadamu nimeyafunika makosa yangu, Kwa kuuficha uovu wangu kifuani mwangu;

34Kwa sababu niliwaogopa mkutano mkubwa, Na dharau la jamaa lilinitia hofu, Hata nilinyamaa kimya, nisitoke mlangoni-

35Laiti ningekuwa na mtu wa kunisikia! (Tazama, sahihi yangu ni hii, Mwenyezi na anijibu); Laiti ningekuwa na hayo mashitaka yaliyoandikwa na adui yangu!

36Hakika ningeyachukua mabegani; Ningejifungia mfano wa kilemba.

37Ningemwambia hesabu ya hatua zangu Ningemkaribia kama vile mkuu.

38Kama nchi yangu yalia juu yangu, Na matuta yake hulia pamoja;

39Kama nimeyala matunda yake pasipo kulipa, Au kama nimewafanya wenyewe kupotewa na uhai;

40Miiba na imee badala ya ngano, Na magugu badala ya shayiri. Maneno ya Ayubu yamekoma hapa.