Ayubu - Sura ya 32

Ayubu - Sura ya 32

1Basi hao watu watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa sababu alikuwa mwenye haki machoni pake mwenyewe.

2Ndipo zikawaka hasira za huyo Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, katika jamaa ya Ramu, juu ya Ayubu, kwa sababu alikuwa amejipa haki mwenyewe zaidi ya Mungu.

3Tena hasira zake ziliwaka juu ya hao rafiki zake watatu kwa sababu hawakupata jawabu, lakini wamemhukumia Ayubu makosa.

4Basi huyo Elihu alikuwa anangoja ili anene na Ayubu, kwa sababu hao wengine walikuwa wazee kuliko yeye.

5Hata Elihu alipoona kuwa hapana jawabu katika vinywa vya watu hao watatu, hasira zake ziliwaka.

6Basi Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, akajibu, na kusema, Mimi ni kijana, na ninyi ni wazee sana; Kwa hiyo nilijizuia, nisithubutu kuwaonyesha nionavyo.

7Nilisema, Yafaa siku ziseme, Na wingi wa miaka ufundishe hekima.

8Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.

9Sio wakuu walio wenye akili, Wala sio wazee watambuao hukumu.

10Basi nilisema, Nisikilizeni mimi; Mimi nami nitawaonyesha nionavyo.

11Tazama, niliyangojea maneno yenu, Nilizisikiliza nisikie hoja zenu, Hapo mlipokitafuta mtakalonena.

12Naam, niliwasikiza ninyi, Na tazama, hapana mmoja aliyemshinda Ayubu, Wala kumjibu maneno yake, kati yenu.

13Jitunzeni msiseme, Sisi tumepata hekima; Mungu yumkini akamshinda, si mtu;

14Kwa kuwa yeye hajayaelekeza maneno yake kwangu; Wala sitamjibu mimi kwa maneno yenu.

15Wameshangaa, hawajibu tena; Hawana neno la kusema.

16Na mimi, je! Ningoje, kwa sababu hawaneni, Kwa sababu wasimama kimya, wala wasijibu tena;

17Mimi nami nitajibu sehemu yangu, Mimi nami nitaonyesha nionavyo.

18Kwa kuwa nimejaa maneno; Roho iliyo ndani yangu hunihimiza.

19Tazama, tumbo langu ni kama divai iliyozibwa; Kama viriba vipya li karibu na kupasuka.

20Nitanena, ili nipate kutulia; Nitafunua midomo yangu na kujibu.

21Tafadhali, nisiupendelee uso wa mtu; Wala sitajipendekeza kwa mtu ye yote.

22Kwani mimi sijui kujipendekeza; Au Muumba wangu angeniondoa kwa upesi.