Ayubu - Sura ya 34

1Tena Elihu akajibu na kusema,
2Sikilizeni maneno yangu, enyi wenye hekima; Tegeni masikio kwangu, ninyi mlio na maarifa.
3Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno, Kama vile kaakaa lionjavyo chakula.
4Na tujichagulie yaliyo ya uelekevu; Na tujue wenyewe yaliyo mema.
5Kwani Ayubu amesema, Mimi ni mwenye haki, Naye Mungu ameniondolea haki yangu;
6Nijapokuwa mwenye haki, nimehesabiwa kuwa mwongo; Jeraha yangu haiponyeki, nijapokuwa sina makosa.
7Je! Ni mtu gani mfano wa Ayubu, Anywaye mzaha kama maji?
8Atembeaye na hao watendao uovu, Na kwenda pamoja na watu wabaya.
9Kwa kuwa amenena, Haimfai mtu lo lote Kujifurahisha na Mungu.
10Kwa hiyo nisikilizeni, enyi wenye fahamu; Mungu asidhaniwe kutenda udhalimu; Wala Mwenyezi kufanya uovu.
11Kwani atamlipa binadamu kwa kazi yake, Naye atamfanya kila mtu kuona sawasawa na njia zake
12Naam, hakika, Mungu hatatenda mabaya, Wala Mwenyezi hatapotosha hukumu.
13Ni nani aliyemwagiza kuiangalia dunia? Au ni nani aliyemwekea ulimwengu huu wote?
14Kama akimwekea mtu moyo wake, Akijikusanyia roho yake na pumzi zake;
15Wenye mwili wote wataangamia pamoja, Nao wanadamu watarejea tena kuwa mavumbi.
16Ikiwa una ufahamu, sikia neno hili; Isikilize sauti ya maneno yangu.
17Je! Atatawala mtu aichukiaye haki hata mmoja? Nawe, je! Utamhukumia mkosa aliye na haki na mwenye nguvu?
18Je! Inafaa kumwambia mfalme, Wewe u mwovu? Au kuwaambia wakuu, Ninyi ni wabaya?
19Sembuse huyo asiyependelea nyuso za wakuu, Wala hawajali matajiri kuliko maskini? Kwani wote ni kazi ya mikono yake,
20Hufa ghafula, hata usiku wa manane; Watu hutikisika na kwenda zao, Nao mashujaa huondolewa pasipo mkono wa mtu.
21Kwani macho yake ya juu ya njia za mtu, Naye huiona miendo yake yote.
22Hapana weusi, wala hilo giza tupu, Wawezapo kujificha watendao udhalimu.
23Kwani yeye hana haja ya kumfikiria mtu zaidi, ili aende mbele za Mungu ahukumiwe.
24Yeye huwavunja-vunja mashujaa pasina kuwachunguza, Na kuwaweka wengine mahali pao.
25Kwa sababu hiyo yeye huyatafiti matendo yao; Naye huwapindia usiku, wakaangamia.
26Yeye huwapiga kama watu wabaya Waziwazi mbele ya macho ya wengine;
27Kwa sababu walikengeuka, wasimwandame yeye, Wasikubali kuzishika njia zake hata moja;
28Hata wakafanya kilio cha maskini kumfikilia, Naye akasikia kilio cha hao wateswao.
29Akitoa utulivu yeye, ni nani awezaye kuhukumia makosa? Akificha uso wake, ni nani awezaye kumtazama? Kama hufanyiwa taifa, au mtu mmoja, ni sawasawa;
30Kwamba huyo mpotovu asitawale, Pasiwe na wa kuwatega watu.
31Kwani kuna mtu aliyemwambia Mungu, Mimi nimevumilia kurudiwa, ingawa sikukosa;
32Nisiyoyaona nifundishe wewe; Kama nimefanya uovu sitafanya tena?
33Je! Malipo yake yatakuwa kama upendavyo wewe, hata ukayakataa? Kwani yakupasa wewe kuchagua, si mimi; Kwa sababu hiyo sema uyajuayo.
34Watu walio na akili wataniambia, Naam, kila mtu mwenye hekima anisikiaye;
35Huyo Ayubu amesema pasipo maarifa, Na maneno yake hayana hekima.
36Laiti Ayubu angejaribiwa hata mwisho, Kwa kuwa amejibu kama watu waovu.
37Kwani huongeza uasi juu ya dhambi zake, Apiga makofi kati yetu, Na kuongeza maneno yake kinyume cha Mungu.