Ayubu - Sura ya 37

Ayubu - Sura ya 37

1Moyo wangu hunitetema kwayo pia, Nao hutoka mahali pake.

2Zisikizeni hizo kelele za sauti yake, Na uvumi utokao kinywani mwake.

3Yeye huituma iende chini ya mbingu zote, Na radi yake hata miisho ya nchi.

4Baadaye sauti hunguruma; Yeye hunguruma kwa sauti ya ukuu wake; Hazizuii hapo sauti yake isikiwapo.

5Mungu hunguruma kwa kustaajabisha kwa sauti yake; Hufanya mambo makuu, ambayo hatuwezi kuelewa nayo.

6Kwani huiambia theluji, Anguka juu ya nchi; Na vivyo manyonyota ya mvua, Na hayo maji ya mvua yake kubwa.

7Huufunga mkono wa kila binadamu; Ili watu wote aliowaumba wajue.

8Hapo wanyama huingia mafichoni, Na kukaa katika mapango yao.

9Dhoruba hutoka katika vyumba vyake; Na baridi ghalani mwake.

10Barafu huletwa kwa pumzi za Mungu; Na upana wa maji huganda.

11Naam, huyatweka mawingu mazito mzigo wa maji; Hulitandika wingu la umeme wake;

12Nalo hugeuzwa huku na huku kwa uongozi wake, Ili yafanye yote atakayoyaagiza Juu ya uso wa dunia hii ikaayo watu;

13Kama ni kwa kuonya, au kama ni kwa nchi yake, Au kama ni kwa rehema, ndiye aletaye.

14Sikiliza neno hili, Ee Ayubu; Simama kimya, uzifikiri kazi za Mungu za ajabu.

15Je! Wajua wewe jinsi Mungu anavyoziagiza, Na kuumulikisha umeme wa wingu lake?

16Je! Wajua jinsi mawingu yalivyowekwa sawasawa, Hizo kazi za ajabu za huyo mkamilifu wa maarifa?

17Jinsi nguo zako zilivyo na moto, Hapo nchi ituliapo kwa sababu ya upepo wa kusini?

18Je! Waweza kuzitandaza mbingu pamoja naye, Ambazo zina nguvu kama kioo cha kuyeyushwa?

19Utufundishe ni maneno gani tutakayomwambia; Kwa maana hamwezi kuyatengeza kwa sababu ya giza.

20Je! Aambiwe kwamba nataka kunena? Au mtu angetamani kumezwa?

21Na sasa watu hawawezi kuutazama mwanga ung'aao mbinguni; Lakini upepo ukipita huzitakasa.

22Kaskazini hutokea umemetufu wa dhahabu; Mungu huvikwa ukuu utishao.

23yeye Mwenyezi hamwezi kumwona; Yeye ni mkuu mwenye uweza; Tena mwenye hukumu, na mwingi wa haki, hataonea.

24Kwa hiyo watu humwogopa; Yeye hawaangalii walio na hekima mioyoni.