Ayubu - Sura ya 38

Ayubu - Sura ya 38

1Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema,

2Ni nani huyu atiaye mashauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa?

3Basi jifunge viuno kama mwanamume, Maana nitakuuliza neno, nawe niambie.

4Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu.

5Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake?

6Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni,

7Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?

8Au ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni.

9Nilipolifanya wingu kuwa vazi lake, Na giza zito kuwa nguo ya kuifungia,

10Nikaiagiza amri yangu; Nikaiwekea makomeo na milango,

11Nikasema, Utafika mpaka hapa, lakini hutapita, Na hapa mawimbi yako yanyetayo yatazuiliwa?

12Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake?

13Yapate kuishika miisho ya nchi, Waovu wakung'utwe wakawe mbali nayo?

14Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, Vitu vyote vinatokea kama mavazi.

15Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, Na mkono ulioinuka huvunjika.

16Je! Umeziingia chemchemi za bahari, Au umetembea mahali pa siri pa vilindi?

17Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu?

18Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote.

19Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi?

20Upate kuipeleka hata mpaka wake, Upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake?

21Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, Na hesabu ya siku zako ni kubwa!

22Je! Umeziingia ghala za theluji, Au umeziona ghala za mvua ya mawe,

23Nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, Kwa siku ya mapigano na vita?

24Je! Nuru hutengwa kwa njia gani, Au upepo wa mashariki hutawanywaje juu ya nchi?

25Ni nani aliyepasua mfereji kwa maji ya gharika, Au njia kwa umeme wa radi;

26Kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu; Juu ya jangwa asiyokaa mwanadamu;

27Kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa, Na kuyameza majani yaliyo mororo?

28Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande?

29Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?

30Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi.

31Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni?

32Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake?

33Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia?

34Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize?

35Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa?

36Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni?

37Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu kwa hekima? Au ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni?

38Wakati mavumbi yagandamanapo, Na madongoa kushikamana pamoja?

39Je! Utamwindia simba mke mawindo? Au utashibisha njaa ya simba wachanga,

40Waoteapo mapangoni mwao, Wakaapo mafichoni wapate kuvizia?

41Ni nani anayempatia kunguru chakula, Makinda yake wanapomlilia Mungu, Na kutanga-tanga kwa kutindikiwa na chakula?