Ayubu - Sura ya 4

Ayubu - Sura ya 4

1Ndipo huyo Elifazi, Mtemani, akajibu na kusema,

2Mtu akijaribu kuzungumza nawe, je! Utaona ni vibaya? Lakini ni nani awezaye kujizuia asinene?

3Tazama, wewe umewafunza watu wengi, Nawe umeitia nguvu mikono iliyokuwa minyonge.

4Maneno yako yamemtegemeza huyo aliyekuwa anaanguka, Nawe umeyaimarisha magoti manyonge.

5Lakini sasa haya yamekufikilia wewe, nawe wafa moyo; Yamekugusa, nawe wafadhaika.

6Je! Dini yako siyo mataraja yako, Na matumaini yako si huo uelekevu wa njia zako?

7Kumbuka, tafadhali, ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? Au hao waelekevu, walikatiliwa mbali wapi?

8Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, Na kupanda madhara, huvuna yayo hayo.

9Kwa pumzi za Mungu huangamia. Na kwa kuvuma kwa hasira zake humalizika.

10Kunguruma kwake simba, na sauti ya simba mkali, Na meno ya simba wachanga, yamevunjika.

11Simba mzee huangamia kwa kukosa mawindo, Nao watoto wa simba mke wametawanyika mbalimbali.

12Basi, nililetewa neno kwa siri, Sikio langu likasikia manong'ono yake.

13Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku, Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu.

14Hofu iliniangukia na kutetema, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote.

15Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama.

16Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake, Mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; Kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena,

17Je! Binadamu atakuwa na haki kuliko Mungu? Je! Mtu atakuwa safi kuliko Muumba wake?

18Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; Na malaika zake huwahesabia upuzi;

19Je! Si zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, Ambazo misingi yao i katika mchanga, Hao waliosetwa mbele ya nondo!

20Kati ya asubuhi na jioni huvunjwa-vunjwa; Waangamia milele wala hapana atiaye moyoni.

21Je! Kamba ya hema yao haikung'olewa ndani yao? Wafa, kisha hali hawana akili.