Ayubu - Sura ya 40

Ayubu - Sura ya 40

1Bwana akafuliza kumjibu Ayubu, na kusema,

2Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi? Mwenye kujadiliana na Mungu, na ajibu yeye.

3Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema,

4Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu.

5Nimenena mara moja, nami sitajibu; Naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.

6Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema,

7Jifunge viuno kama mwanamume, Mimi nitakuuliza neno, nawe niambie.

8Je! Hata hukumu yangu utaibatilisha? Utanitia mimi hatiani, upate kuhesabiwa haki?

9Au je! Wewe una mkono kama Mungu? Waweza kutoa ngurumo kwa sauti kama yeye?

10Haya! Jivike sasa fahari na ukuu; Jipambe heshima na enzi.

11Mwaga mafuriko ya hasira zako, Ukamtazame kila mtu mwenye kiburi, ukamdhili.

12Mtazame kila mtu mwenye kiburi ukamshushe, Ukawakanyage waovu hapo wasimamapo.

13Wafiche mavumbini pamoja, Wafunge nyuso zao mahali palipositirika.

14Ndipo mimi nami nitazikiri habari zako, Ya kuwa mkono wako wa kuume waweza kukuokoa.

15Mwangalie huyo kiboko, niliyemwumba pamoja nawe; Yeye hula nyasi kama vile ng'ombe,

16Tazama basi, nguvu zake ni katika viuno vyake, Na uwezo wake u katika mishipa ya tumbo lake.

17Yeye hutikisa mkia wake mfano wa mwerezi; Mishipa ya mapaja yake yanaungamana pamoja.

18Mifupa yake ni kama mirija ya shaba; Mbavu zake ni kama vipande vya chuma.

19Yeye ni mkuu wa njia za Mungu; Yeye aliyemfanya alimpa upanga wake.

20Hakika milima humtolea chakula; Hapo wachezapo wanyama wote wa barani.

21Hulala chini ya miti yenye vivuli, Mafichoni penye mianzi, na matopeni.

22Hiyo miti yenye vivuli humfunika kwa vivuli vyao; Mierebi ya vijito humzunguka.

23Tazama, mto ukifurika, yeye hatetemeki; Hujiona yu salama, ijapokuwa Yordani hufurika hata kinywani pake.

24Je! Mtu ye yote atamnasa akiwa yu macho, Au, kumtoboa pua yake kwa mtego?