Ayubu - Sura ya 5

Ayubu - Sura ya 5

1Haya, ita sasa; je! Yuko atakayekujibu? Nawe utamwelekea yupi katika hao watakatifu?

2Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga.

3Nimewaona wapumbavu wakishusha mizizi; Lakini mara niliyalaani maskani yake.

4Watoto wake wako mbali na wokovu, Nao wamesongwa langoni, Wala hapana atakayewaponya.

5Mavuno yake wale wenye njaa huyala, Na kuyatwaa hata kuyatoa miibani, Nao wenye kiu huzitwetea mali zao.

6Kwani taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi;

7Lakini mwanadamu huzaliwa ili apate mashaka, Kama cheche za moto zirukavyo juu.

8Lakini mimi ningemtafuta Mungu, Ningemwekea Mungu daawa yangu;

9Yeye afanyaye mambo makuu, yasiyotambulikana; Mambo ya ajabu yasiyo na hesabu;

10Yeye atoaye mvua inyeshe juu ya nchi, Na kuyapeleka maji mashambani;

11Awainuaye juu hao walio chini; Na hao waombolezao hukuzwa wawe salama.

12Yeye huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao.

13Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao wenyewe; Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka.

14Wao hupatwa na giza wakati wa mchana, Hupapasa mchana vilevile kama usiku.

15Lakini yeye huokoa na upanga wa kinywa chao, Hata kumwokoa mhitaji na mkono wake aliye hodari.

16Basi hivi huyo maskini ana matumaini, Na uovu hufumba kinywa chake.

17Tazama, yu heri mtu yule Mungu amwadhibuye; Kwa hiyo usidharau kurudiwa na huyo Mwenyezi.

18Kwani yeye huumiza, lakini tena huuguza; Yeye hutia jeraha, na mikono yake huponya.

19Yeye atakuokoa na mateso sita; Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa.

20Wakati wa njaa atakukomboa na mauti; Na vitani atakukomboa na nguvu za upanga.

21Utafichwa na mapigo ya ulimi; Wala usiogope maangamizo yatakapokuja.

22Wewe utayacheka maangamizo na njaa; Wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi.

23Kwani utakuwa na mapatano na mawe ya bara; Nao wanyama wa bara watakuwa na amani kwako.

24Nawe utajua ya kwamba hema yako ina salama; Na zizi lako utaliaua, wala usikose kitu.

25Tena utajua ya kwamba uzao wako utakuwa mwingi, Na vizazi vyako watakuwa kama nyasi za nchi.

26Utafika kaburini mwenye umri mtimilifu, Kama mganda wa ngano ulivyo wakati wake.

27Tazama, haya tumeyapeleleza, ndivyo yalivyo; Yasikie, uyajue, ili upate mema.