Ayubu - Sura ya 7

Ayubu - Sura ya 7

1Je! Mtu hana wakati wake wa vita juu ya nchi? Na siku zake, je! Si kama siku za mwajiriwa?

2Kama mtumishi atamaniye sana kile kivuli, Kama mwajiriwa anayetazamia mshahara wake;

3Ni vivyo nami nimepewa miezi ya ubatili iwe fungu langu, Nami nimeandikiwa masiku yenye kuchokesha.

4Hapo nilalapo chini, nasema, Nitaondoka lini? Lakini usiku huwa mrefu; Nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke.

5Mwili wangu unavikwa mabuu na madongoa ya udongo; Ngozi yangu hufumba, kisha ikatumbuka tena.

6Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia, Nazo zapita pasipokuwa na matumaini.

7Kumbuka ya kwamba maisha yangu ni upepo; Jicho langu halitaona mema tena.

8Jicho lake huyo anionaye halitaniangalia tena; Macho yako yatanielekea, lakini sitakuwapo.

9Kama vile wingu likomavyo na kutoweka, Ni vivyo huyo ashukaye kuzimuni hatazuka tena kabisa.

10Hatarudi tena nyumbani kwake, Wala mahali pake hapatamjua tena.

11Kwa hiyo sitakizuia kinywa changu; Nitanena kwa mateso ya roho yangu; Nitalia kwa uchungu wa nafsi yangu.

12Je! Mimi ni bahari, au je! Ni nyangumi? Hata ukawaweka walinzi juu yangu?

13Hapo nisemapo, kitanda changu kitanituza moyo, Malazi yangu yatanipunguzia kuugua kwangu;

14Ndipo unitishapo kwa ndoto, Na kunitia hofu kwa maono;

15Hata nafsi yangu huchagua kunyongwa, Na kuchagua kifo kuliko maumivu yangu haya.

16Ninadhoofika; sitaishi sikuzote; Usinisumbue, kwani siku zangu ni uvuvio.

17Je! Mtu ni kitu gani, hata ukamtukuza, Na kumtia moyoni mwako,

18Na kumwangalia kila asubuhi, Na kumjaribu kila dakika?

19Je! Hata lini hukomi kuniangalia; Wala kunisumbua hata nimeze mate?

20Kwamba nimefanya dhambi, nikufanyieje Ee mlinda wanadamu? Mbona umeniweka niwe shabaha yako, Hata nimekuwa mzigo kwa nafsi yangu?

21Nawe, je! Mbona hunisamehe makosa yangu, Na kuniondolea maovu yangu? Kwa kuwa sasa nitalala mavumbini; Nawe utanitafuta kwa bidii, lakini sitakuwapo.