Yohana - Sura ya 10

Yohana - Sura ya 10

1Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi.

2Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo.

3Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje.

4Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake.

5Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni.

6Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia.

7Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo.

8Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia.

9Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.

10Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

11Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

12Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.

13Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.

14Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi;

15kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.

16Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.

17Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.

18Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.

19Kukaingia tena matengano kati ya Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo.

20Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza?

21Wengine wakasema, Maneno hayo siyo ya mtu mwenye pepo. Je! Pepo aweza kuwafumbua macho vipofu?

22Basi huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi.

23Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani.

24Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi.

25Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia.

26Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu.

27Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.

28Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu.

29Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.

30Mimi na Baba tu umoja.

31Basi Wayahudi wakaokota mawe tena ili wampige.

32Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?

33Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.

34Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?

35Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka);

36je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu?

37Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini;

38lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.

39Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao.

40Akaenda zake tena ng'ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohana akibatiza hapo kwanza, akakaa huko.

41Na watu wengi wakamwendea, wakasema, Yohana kweli hakufanya ishara yo yote, lakini yote aliyoyasema Yohana katika habari zake huyu yalikuwa kweli.

42Nao wengi wakamwamini huko.