Yohana - Sura ya 21

1Baada ya hayo Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi.
2Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja.
3Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu.
4Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu.
5Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La.
6Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki.
7Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini.
8Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki.
9Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate.
10Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi.
11Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka.
12Yesu akawaambia, Njoni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana.
13Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo.
14Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu.
15Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda
16Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu.
17Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.
18Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.
19Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate.
20Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?)
21Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je?
22Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi.
23Basi neno hilo lilienea katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe?
24Huyu ndiye yule mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya: nasi twajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.
25Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.